Kampuni ya mawasiliano ya Smile Telecom nchini Uganda imeamua kuwalipia kodi ya kila siku ya shilingi 200 za Uganda kwa wateja wake wote kwa muda wa miezi mitatu ili waweze kutumia mitandao ya kijamii.
Serikali ya Uganda kuanzia Julai Mosi mwaka huu imeanza kulipisha wananchi wake wote kodi kwa kila mwenye kutaka kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, Facebook, Twitter, Google Hangouts, Yahoo Messenger, Instagram, YouTube, Skype na mingine.
Taarifa ya Smile Telecom kwa wateja wake imesema kwamba wateja wake wanapaswa kuendelea kununua kifurushi cha intaneti kama kawaida na kwamba hakutakuwa na hatua za usajili za kulipia kodi kwa ajili ya mitandao ya kijamii.
Meneja wa masoko wa Smile, Felix Owilo amesema kampuni yake inataka wateja wao wapate huduma za intaneti zilizo kamili ikiwemo ya kutumia mitandao ya kijamii bila ya usumbufu wowote.
Smile Telecom katika juhudi za kuunga mkono serikali ya Uganda kukusanya kodi wameona ni vyema jukumu hilo walichukue wao ili kusaidia ulipaji kodi pamoja na kumpunguzia uzito mwananchi wa kawaida.