Elon Musk ni moja ya watu maarufu zaidi duniani ambao wanamatumizi makubwa ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Uamuzi wake wa kutaka kununua kampuni hiyo na kuiondoa toka kwenye soko la hisa umeleta mazungumzo mengi mtandaoni – ya kupinga na mengine ya kuunga mkono.
Elon Musk ni nani?
Elon Musk ni mfanyabiashara mkubwa aliyepata umaarufu kupitia ubunifu na mafanikio makubwa kwenye biashara za magari ya umeme yenye uwezo wa kujiendesha yenyewe ya Tesla, na kampuni ya roketi za anga za juu zenye uwezo wa kutua zenyewe, Space X. Hizi ni baadhi tu ya biashara zilizompa umaarufu, kumfahamu zaidi soma makala yetu hapa (Bofya).
Elon Musk na mpango wa kununua Twitter
Mapema mwaka huu Bwana Elon aliaanza kuuliza maswali mbalimbali kupitia akaunti yake ya Twitter kuonesha kana kwamba mtandao huo unahitaji mageuzi. Mageuzi ya kiutaratibu, pamoja na mageuzi yanayolenga kuongeza uhuru na kutozuia maoni ya baadhi ya watu kwenye mtandao huo. Mmoja wa waanga wa kufungiwa akaunti zao kutokana na maoni yao ni Rais aliyepita wa Marekani, Rais Trump.
Given that Twitter serves as the de facto public town square, failing to adhere to free speech principles fundamentally undermines democracy.
What should be done? https://t.co/aPS9ycji37
— Elon Musk (@elonmusk) March 26, 2022
Wiki chache zilizopita Bwana Musk aliweka wazi kwamba mapema mwaka huu alinunua hisa za kampuni ya Twitter na kumfanya kuwa mmoja kati ya wamiliki wakubwa wa kampuni hiyo – kwa asilimia 7.
Kilichofuata baada ya hapo:
- Bodi ilimualika kujiunga, na kuwa mmoja kati ya bodi ya usimamizi ya uendeshaji wa kampuni hiyo
- Inaonekana moja ya utaratibu kwa wale wanaoketi kwenye bodi ni kuwazuia kuongelea vibaya au kutoa changamoto dhidi ya kampuni hiyo nje ya vikao vya bodi
- Bwana Musk hakutaka kubanwa na utaratibu huu, hivyo akakataa ofa hiyo ya kuketi kwenye bodi
- Akachagua kutoa ofa ya moja kwa moja ya kutaka kununua hisa zote za kampuni hiyo, na kuitoa kwenye soko la hisa – kuifanya kuwa kampuni binafsi.
- Anaamini kwa kufanya hivyo ndio ataweza kuwa huru kufanya marekebisho na maboresho ya kimfumo na kiutendaji katika kampuni hiyo
Jambo hili limeleta hisia tofauti kwa wadau mbalimbali. Wapenda uwepo wa uhuru zaidi wa kimawazo kwenye mtandao huo wameonesha kuunga mkono ofa ya Bwana Musk. Ofa ambayo atanunua hisa kwa bei ya juu kuliko wastani wa thamani za hisa hizo za sasa na kabla ya yeye kuweka wazi taarifa za umiliki wake.
Wapo pia wanaopinga wakimuona Bwana Musk kama mtu asiyetabirika, na hivyo kuwa na wasiwasi juu ya jinsi mabadiliko anayotaka yaje yatawapa nafasi watu wasiopenda kwenye mtandao huo kuwa huru zaidi.
Kwa sasa kwa asilimia kubwa inaonekana Bwana Musk atafanikiwa, ingawa tayari imeonekana bodi ya kampuni hiyo inatamani kutomuwezesha Bwana Musk kukamilisha hitaji lake. Ila bodi hiyo haina nguvu sana, kwani kwa asilimia kubwa wote hawana umiliki mkubwa wa hisa katika kampuni hiyo.
No Comment! Be the first one.