Kutana na Freedom 251 – Simu janja ya bei rahisi zaidi duniani! Hakika kwa sasa hakuna mshindani wa bei wa simu janja hii kutoka kampuni moja huko nchini India.
Simu ya Freedom 251 iliyotambulishwa na kuanza kuuzika kwa bei ya chini ya Tsh 8,000/= | Ksh 410 ilisababisha hadi mtandao wa kampuni iliyoitengeneza kushindwa kuhimili watumiaji mamilioni walioutembelea mara moja ili kuweza kujipatia simu hiyo.
Freedom 251 imetengenezwa na nani?
Simu janja hii ya Freedom 251 imetengenezwa na kampuni mpya tuu isiyo na ata miaka miwili katika biashara ya utengenezaji na uuzaji wa simu – Ringing Bells iliyopo katika jimbo la Uttar Pradesh huko nchini India. Bei yake ni rupee 251 ambayo ni takribani dola 3.6 za kimarekani.
Ina sifa gani?
- Inakuja na toleo la Android 5.1 Lollipop
- Kamera ya selfie ya megapixel 0.3 na ile kuu ikiwa ni ya megapixel 3.2
- Inakubali teknolojia za 2G na 3G pamoja na WiFi
- Ina betri la mAh 1450
- Kioo (display) cha sentimita 10
- Prosesa ya 1.3GHz quad-core
- RAM ya GB 1 pamoja na diski uhifadhi (storage) wa GB 8 – unaweza kutumia memori kadi (SD Card) ya hadi GB 32
Pia inakuja na apps muhimu kama vile Google Play, WhatsApp, Facebook, YouTube na zingine muhimu kwa watumiaji wa nchini India.
Inasemekana vitu muhimu (components) katika simu hiyo wanavinunua kutoka Taiwan. Wengi wanajiuliza kampuni hiyo inawezaje kutengeneza faida kwa bei yao hii, wengi wanaona simu hiyo inatakiwa iuzwe kwa bei ya si chini ya dola 50 za Kimarekani.
Ili kuondoa gharama zaidi kampuni hiyo inauza simu hiyo kupitia mtandao wao tuu. Simu hiyo imetambulishwa Alhamisi wiki hii na tayari imejipatia umaarufu duniani kote. Watu waliopo nchini India wanaweza kununua simu hiyo kupitia www.freedom251.com na simu zitaanza kutumwa kuanzia mwezi wa sita.
Tayari kuna dalili kampuni ikawa inajiingiza kwenye matatizo kwani kuna wizi wa kiubunifu unaonekana umefanyika hasa hasa kwa kuiga muonekano wa simu za iPhone…lakini bado kampuni ya Apple haijazungumza chochote.
Bado haijajulikana kama simu hiyo itaweza kupatikana duniani kote, na ata kama ikiwa hivyo basi bei itapanda kidogo kwa ajili ya usafirishaji pamoja na faida za wafanyabiashara – ila ata gharama hizo zikiongezeka bado inaonekana simu janja hii itaendelea kuwa ni ya bei ya chini sana.
No Comment! Be the first one.