Huko jijini Barcelona kampuni ya Samsung imetambulisha simu iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu sana. Hapo jana wametambulisha rasmi Samsung Galaxy S6 na Galaxy S6 Edge.
Jambo kubwa sana ni kwamba toleo la Galaxy S6 limebadilisha kabisa muonekano wa familia za simu za Galaxy S kulinganisha na zilizopita. Mambo makubwa yamefanyika katika kuleta uhai mpya kwa familia ya simu hizi maarufu duniani. Inawezekana ikawa ni mapema kusema ila inaonekana iPhone 6 zimepata ushindani wa kwelikweli hapa.
Kioo
Kwanza kabisa kwenye suala la ubora wa kioo muonekano (display) simu hizi ni za inchi 5.1 zikiwa zimebeba moja ya kiwango kikubwa zaidi cha HD iliyokamilika ya 1080x1920p. Pia kupitia teknolojia ya SuperAMOLED iliyotumika tegemea kiwango cha juu kabisa cha muonekano.
Katika toleo la Galaxy S6 Edge kioo kimesogea kufunika pande mbili za pembeni (Edge), ila wengi wamekosea uwepo wa pande zote mbili kwani kila wakati utaweza kuutumia upande mmoja tuu. Eneo hili ambalo kwenye toleo la Galaxy Note Edge lilikuwa upande mmoja tuu linaweza kutumika kwa ajili ya kupata taarifa muhimu (notifications) kwa urahisi zaidi. Na hadi sasa wengi wamedai eneo ilo halina uwezo wa kazi nyingi zaidi kama ilivyokuwa kwa Galaxy Note Edge.
Je kwenye ubunifu kuna lolote jipya?
Ndio! Baada ya malalamiko ya wengi toleo ili la Galaxy S vazi (housing) lote limetumia chuma na vioo na kuachana kabisa na masuala ya plastiki. Pia kama kawaida ya simu janja nyingi za kiwango cha juu utaweza kuondoa ‘screen lock’ kwa kupitisha kidole tuu kwenye sensa zilizopo kwenye sehemu ya kubofya ‘Homescreen’.
Sifa moja kubwa kiubunifu inabakia kuwa uamuzi wa kuachana utumiaji wa plastiki.
Je programu uendeshaji ipo vipi?
Kubwa zaidi ni uamuzi wa Samsung kupunguza apps na mambo mengine mengi ambayo hayakuwa ya msingi kwenye programu yao ya TouchWiz ambayo inajengwa juu ya toleo jipya kabisa la Android Lollipop, yaani Android 5.0. Imejitaidi kutopoteza mambo mengi yanayopatikana katika toleo hili la Android linalokuja na muonekano mzuri wa kiubunifu kutoka Google – yaani Material Design. Kusoma zaidi kuhusu Material Design – BOFYA HAPA!
TeknoKona tunaamini uamuzi huu wa kupunguza apps zisizokuwa za msingi utasaidia sana kuepusha utumiaji wa chaji usio wa kilazima na pia kuipa RAM uhuru zaidi kwa ajili ya matumizi mengine.
Je zile sifa zaidi ni zipi?
Iwe S6 au S6 Edge zote utapata prosesa ya 2.1GHz octa-core na GB 3 za RAM
Kiwango hichi cha RAM pamoja na prosesa ni kikubwa na kitakachofanya simu hizi kuwa haraka sana bila wasiwasi uzito kiutendaji.
Je utaweza kutumia MicroSD? Hapana! Majanga!
Kama wafanyavyo Apple katika iPhone Samsung nao wameamua kuondoa uwezo wa utumiaji wa kadi za SD ila wanakupa uchaguzi wa kununua simu yenye uwezo wa diski uhifadhi wa GB 32, 64 au 128! Na Samsung wamesema wametumia teknolojia mpya katika kutengeneza diski uhifadhi hizo na hivyo ufanyaji kazi wake ni zaidi ya asilimia 80% bora zaidi kuliko teknolojia inayotumika kwenye simu nyingi kwa sasa.
Betri je? Ni 2,600mAh!
Hichi ni kiwango kidogo ikilinganishwa na betri iliyo kwenye toleo lililopita, yaani Galaxy S5. Samsung wanadai usihofu kuhusu ili kwani wametumia teknolojia inayofanya kuchaji kiwango cha betri kikiwa sifuri hadi kufika mia, yaani kujaa, ndani ya dakika 30 hadi 40 tuu.
Wazee na mabinti wa ‘selfies’ inakuwaje?
Kwenye eneo la kamera Samsung wanadai wamejikita katika kuzidi kuongeza uwezo wa simu hiyo kupiga picha katika giza/mwanga mdogo. Kamera yake ya nyumba itakuwa na kiwango kikubwa tuu cha MP (Megapixels) 16, wakati kamera ya mbele ya kioo kwa ajili ‘Selfies’ inauwezo wa MP 5.
Wengi wanaona kampuni ya Samsung imejitahidi kuleta simu zenye kiwango kikubwa na cha kuweza kuleta ushindani sokoni. Na mafanikio ya simu hizi yanaweza yakawa ni baraka kubwa kwa kampuni hiyo kwani kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikiona faida zake zikizidi kushuka kiasi cha kupitwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Apple.
Je umevutiwa na simu hizi? Tueleze, Ungana nasi pia kupitia Twitter, Facebook na Instagram
dah kiukweli ulimwengu wa Samsung ndo wenyew maan kila kona wapo vizuri mno. keep it up