Kampuni ya Google imetangaza ujio wa programu yao mpya ya uendeshaji iitwayo ‘Android L’ kwa sasa. Tutegemee jina kamili hapo baadae ila kwa kuangalia utamaduni wa Google wa kuita programu zake za uendeshaji kwa majina ya aina ya vyakula, keki na ata aisikrimu basi tutegemee L kuwakilisha kitu flani kama ‘Lollipop’ au kingine chochote.
Kikubwa kakubwa zaidi katika Android L ni kama ifuatavyo:
Ujio wa ‘Material Design’
Wakati kampuni nyingi za vifaa vya elektroniki kama Apple kupitia iOS na Microsoft kupitia Windows OS wanaungana na mitandao mingi katika kutumia ubunifu (design) maarufu kwa sasa ya ijulikanayo kama ‘Flat design’, Google amekuja na muundo mpya ambapo amechukua sifa nzuri za muundo wa ‘Flat design’ na kuja na kitu kijulikanacho kama ‘Material Design’. Angalia picha chini kujionea tofauti kati ya ubunifu wa kawaida, wa ‘Flat design’ na huu mpya wa Material design.
Na hapa angalia muunekano wa Android L katika ubunifu wa ‘Material’ – Vitu vinaonekana katika uhalisia zaidi kwa kuhusisha uhalisia flani. Ukitaka kuona vizuri jinsi gani ubunifu huu ulivyo tembelea mtandao maalumu wa Google Design kwa kubofya hapa!
UI – Kimuonekano Android L inavutia zaidi, ‘Material design’ imeambatana na tabia mbalimbali za kuvutia pale unapobofya/kugusu sehemu au kitu flani. Muonekano huu unakuwa unaendelea kuonekana vilevile bila kujarisha aina ya kifaa unachotumia- Simu, Kompyuta au Tableti. Kutakuwa na utofauti flani unajitokeza pale unapogusa au kufungua sehemu, hii ni pamoja rangi tofauti kujitokezea au ata ‘animations’ flani.
Sehemu ya Kukupa Notisi ((Notifications’)
Simu itakapokuwa imefungwa utaweza kuona taarifa/notisi mbalimbali hii ni pamoja na kukupa uwezo wa kufungua habari husika au kuipotezea (Swipe) iondoke kwenye notisi. Sehemu ya notisi/taarifa imeumuishwa na skrini-fungwa (lockscreen), hii ni katika kukusaidia kuweza kufahamu kama umepokea habari muhimu au la, na kukupa uwezo wa kubofya kutoa kifungo(password) na moja kwa moja utapelekwa kwenye habari/programu husika bila wewe kubofya kingine chochote.
Uwezo wa Kufanya Mengi kwa Wakati Mmoja (Multitasking) pamoja na Mitandao
Kuna ile sehemu ambayo ukibofya katika simu yako ya android inakuwezesha kuona programu mbalimbali ambazo bado unazitumia kwa wakati mmoja, ukiangalia vizuri utagundua kama umefungua programu ya kutumia mtandao kama vile Chrome basi nayo huwa inaonekana pale. Katika Andoid 5 kwa jina lingine Android L utakuwa na uwezo wa kuona kurusa/mitandao husika pia katika orodha hiyo badala ya Chrome. Kwa mfano umefungua mtandao wa Teknokona, Jamii Forums, Michuzi pamoja na mingine kwenye Chrome na pia umefungua programu zingine kama kamera au magemu basi utakapobofya sehemu ya kukuonesha programu zilizowazi utaona pia ile mitandao ipo kwenye orodha pamoja na programu zako zingine na hivyo kukupa uwezo wa kwenda moja kwa moja kwenye mtandao husika. Hii ni tofauti na sasa ambapo unaona Chrome tu na si mitandao uliyofungua katika orodha hiyo.
Vipi Kuhusu Chaji?
Moja ya kitu kinachowauzi wengi linapokuja suala la simu-janja (smartphones) ni suala la kuishiwa na chaji haraka. Kwenye Android L Google wanaleta kitu kipya katika kukusaidia pale unapotaka kupunguza matumizi ya chaji kutokana na programu zisizokuwa za msingi au kipaumbele. Kupitia ‘Project Volta’ Android L itakuwa na sehemu katika mipangilio ambapo utaweza kuchagua mipangilio (settings) flani ambayo itakuwa na uwezo wa kuongeza hadi dakika 90 kutegemea na mipangilio utakayochagua. Itakupa uwezo wa kufahamu programu zinazotumia chaji zaidi na hivyo kukupa uwezo wa kusimamisha utendaji wake kupitia mipangilio hiyo.
Mengineyo?
Katika kukuza uwezo wa kimuonekano (graphics) ili kuboresha muonekano na utendaji wa programu kama magemu na nyinginezo kupitia toleo la Android L Google kwa kushirikiana na Nvidia wametengeneza kitu kinachofahamika kama AEP ambapo ni mjumuhisho wa viprogramu mbalimbali vinavyosaidia kufanya kazi na OpenGL ES katika kuboresha muonekano zaidi. Kwa wale wanaopenda magemu basi hii ni habari njema zaidi, jiandae kuona magemu katika muonekano/uhalisia mzuri zaidi.
No Comment! Be the first one.