Google wamesema wamefanya uamuzi wa kuchelewa kuruhusu apps mpya kuanza kupatikana kwenye Google Play Store kwa sababu za kiusalama.
Soko la apps la Google Play Store ndio soko rasmi la upatikanaji wa mamilioni ya apps za bure na za kununua. Kwa muda mrefu kumekuwa na lawama kuwa ni soko ambalo si salama sana ukilinganisha na soko la apps la App Store kwenye simu za iPhone.
Sababu kuu ikiwa kuna upatikanaji wa apps ambazo zinaweza zikawa na matangazo yanayoharibu kabisa utumiaji wa simu au pia kuwa na apps ambazo zikishawekwa kwenye simu zinakuwa na lengo la kufanya mambo mengine kinyume na taarifa rasmi ya app husika.
Kikawaida imekuwa ikiwachukua Google ndani ya masaa 24 kuruhusu maombi ya apps mpya kuwekwa kwenye Google Play Store.
- Kwa sasa Google wamesema itachukua siku 3 kwa apps mpya kuruhisiwa kwenye soko hilo la apps.
- Muda huu ni kusaidia kufanya uchunguzi mpana zaidi kuhusu app husika na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa Google Play Store.
Tayari Google walishafanya mambo mengi kuhakikisha usalama katika soko hilo, na tayari kulikuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa. Uamuzi huu unalenga kuhakikisha wanafikia kiwango cha asilimia 100.
Google hawataishia kwa apps mpya tuu, bali ata katika masasisho mapya (updates) wanalenga kuweka utaratibu wa kuchunguza masasisho kabla ya kuyaruhusu katika Google Play Store – ila itachukua muda mchache ukilinganisha na apps mpya.