Wengi tunatumia muda mwingi kusoma habari mpya kupitia simu au tableti zetu. Siku hizi unaweza usiende kununua gazeti lakini ukaweza kupata habari kadhaa kupitia simu yako, lakini ni kitu kisichokuwa na ubishi kuna vingi utavikosa. Pia wengi tumeamua kutafuta habari hizo mitandaoni kwa sababu shughuli nzima ya ununuaji na ushikaji wa gazeti mkononi limekuwa si la kuvutia na la urahisi ukilinganisha na kusoma habari yako kwenye simu au tableti yako. Kwa kifupi ni rahisi sana kupoteza ata gazeti ulilonunua dakika chache zilizopita baada ya wewe kuzunguka zunguka kidogo, lakini si rahisi wewe kuacha kutokubeba simu yako mara zote.
Kampuni ya masuala ya kidigitali ya Tanzania, SmartCodes, imetambulisha rasmi app mahususi kwa ajili ya usomaji wa magazeti ya kitanzania. App hiyo waliyoipa jina la M-Paper bado ipo katika kiwango cha ‘beta’, yaani unaweza kutumia lakini maboresho bado yanaendelea na tegemea vijimambo vidogo kutokuwa sawa.
Kupitia M-Paper utaweza kuona magazeti katika uhalisia wake, utaweza kusoma kurasa za mbele na kununua/kulipia kuweza kusoma gazeti zima.
Lakini pia ukishajiandikisha unapatiwa Tsh 10,000/= ya kuanzia ili kukuwezesha kujaribu teknolojia hii.
Tumeijaribu app hii na hadi sasa inafanya kazi vizuri ingawa pia bado ina matatizo madogo madogo yanayojitokeza, magazeti yanaonekana kwa muonekano mzuri na unaweza kusoma bila shida yeyote. Unaweza kujiandikisha kwa urahisi na utaitaji kuwa na barua pepe, jina lako pamoja na nywila (password) uipendayo.
Je unaweza kulipia magazeti kwa njia gani?
Unaweza kulipia magazeti na kuyasoma katika simu yako kwa njia za M-Pesa, Airtel Money, Tigo Pesa, PayPal, pamoja na kadi za Visa au MasterCard.
Itilafu tulizokutana nazo:
App hii bado ipo katika ubora wa beta na hivyo ni sawa kukutana na matatizo madogo madogo, na jinsi yanavyojitokeza ndio watengenezaji wake wanazidi kufanya maboresho zaidi.
- Wakati tushafungua akaunti na kuingia na kujaribu kufungua gazeti app hiyo ilijifunga ghafla. Kurudi tena ikataka kuingiza barua pepe na nywila tena, ata baada ya kuingiza iliyo sahihi bado iliikataa.
- Ukienda chaguo la ‘Forgot Password’, yaani kusahau nywila, ata baada ya kuingiza barua pepe iliyo sahihi ukibofya kukubali app hiyo inashindwa pia kutuma taarifa husika (‘error on Send EMailCloud not instantiate mail function).
Pakua app hii na wewe utuambie umeionaje, ila kwa kiasi kikubwa tunawasifu SmartCodes kwa ubunifu na utengenezaji wa app hii. Inamuonekano mzuri na ni rahisi sana kwa mtu yeyote kufuata hatua chache katika kutengeneza akaunti na ata kuitumia. Katika nchi nyingi ambazo matumizi ya simu/tableti janja yapo juu, watu wangi wanapata magazeti yao kwa njia za dijitali, na huko ndipo Tanzania pia inaelekea.
Faida ya magazeti ya kimtandao ni urahisi wake wa kupatikana, pia urahisi wa uhifadhi. Je wewe unamaoni gani kuhusu utumiaji wa teknolojia kama hizi za apps katika uuzaji wa magazeti? Tuambie, pia kumbuka kupakua app ya M-Paper kutoka Google Play na utuambie maoni yako – M- Paper | Google Play
No Comment! Be the first one.