Kampuni ya Apple na Google kushirikiana katika utengenezaji wa teknolojia ya kufuatilia watu wenye maambukizi ya Coronavirus.
Teknolojia ambayo Google na Apple wanaifanyia kazi na wameshapendekeza kwa serikali ya Marekani na Umoja wa Ulaya utatumia teknolojia ya bluetooth pamoja na intaneti kuwezesha watu kupata taarifa kama mtu au watu waliokutana nao hivi karibuni wana maambukizi ya Coronavirus.
Kwa kufanya hivi basi watu wataweza kupata huduma za afya mapema na pia kuweza kufanya maamuzi ya kuepuka kuwaambukiza wengine.
Jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi;
- Amina na Amani wamekutana sehemu, na wakapiga stori wakiwa wamekaribiana. Au walikuwa kwenye daladala na wamekaa karibu.
- Simu zao kupitia teknolojia ya bluetooth zitatumia namba ya siri.
- Mfano baada ya siku moja au tano Amani akaenda kupima na kukutwa ana maambukizi ya Corona-19, kutakuwa na app kwenye simu yako atatakiwa kutoa taarifa ya kwamba ana maambukizi ya Corona-19.
- App hiyo haitachukua jina lake wala taarifa yake yeyote bali itatuma ile namba ya siri ambayo ilitumwa kwa Amina siku ile, namba hiyo itatumwa kwenda kwenye mtandao.
- Simu ya Amina nayo itakuwa mara kwa mara inadownload taarifa za namba za siri kutoka kwenye mtandao na simu yenyewe itakuwa inahakiki kama kuna mtu Amina alikuwa naye karibu hivi karibuni kama amepata maambukizi.
- Ile namba siri kutoka kwenye simu ya Amani ikitambuliwa na simu ya Amina basi moja kwa moja Amina atapata notification/taarifa fupi ikimwambia kuna mtu aliyekuwa naye karibu hivi karibuni amepimwa na kutambulika ana maambukizi ya COVID-19. Kwa taarifa hii Amina atashauriwa kujiweka karantini au kutafuta huduma za upimaji kama ameanza kuumwa.
Lengo la Google na Apple ni kuifanya teknolojia hiyo kuingia kwenye simu zinazotumia programu endeshaji zao – Android na iOS. Na watawawezesha watengenezaji apps kuweza kutengeneza apps husika kwa nchi husika.