Kampuni za Apple na Google zimekuwa zikitawala anga za kiteknolojia kwa muda mrefu sasa, hasa katika soko la programu za simu za mkononi. Moja ya mada kubwa zilizozuka katika siku za karibuni ni uwezekano wa kampuni hizi mbili kuunga mafanikio yao kwenye soko la vitumi vya mkononi na soko la kompyuta. Kwa kifupi, kampuni hizi zina mtazamo tofauti kabisa juu ya suala hili.
Tim Cook, mtendaji mkuu wa Apple Inc. anasema, kampuni yake inaona kwamba kompyuta na vitumi vya mkononi ni vitu viwili tofauti na uwezekano wa mtumiaji kuridhika na utumiaji sawa sawia kwa simu za mkononi na kompyuta ni kitu ambacho hawana maono nacho kwa sasa. Apple wanaona kwamba kujaribu kuziunga iOS na Mac, kutaleta hisia hasi ya utumiaji kwa pande zote mbili – mtumiaji hataweza kufurahia kifaa chake ipasavyo kama ilivyo sasa hivi.
Kwa upande mwingine, mtendaji mkuu wa kampuni ya Google, Eric Schmidt amezungumza kwenye tamasha la TechCrunch Beijing ya kwamba upo uwezekano wa kuunga programu-endeshaji ya androidi ya vitumi vya mkononi na ile ya ChromeOS kwa ajili ya kompyuta pakato na PC katika siku za karibuni. Schmidt hakusema kiundani kwamba Google watafanya nini kuunganisha ChromeOS na Android na aliamua kuacha watu wenye shauku ya kujua hilo wangojee kuona nini kitatokana na juhudi hizo.
Wakiziungumzia juu ya ni lini tutegemee muungano wa Android na ChromeOS, vyanzo kutoka Google vilivyokaririwa na Wall Street Journal, wanasema kwamba hawana muda maalumu wanaoweza kuutamka kwa umma. Hatahivyo, wachambuzi wanategemea harakati hizo za Google zinaweza kuzaa matunda ndani ya miezi 18.
Wataalamu mbalimbali wanakubaliana na Tim Cook, kwamba yuko sawa kwa sababu programu-endeshaji za iOS na Mac OS zilivyo sasa ni tofauti sana ki-undani (kwenye ‘code’ zake) ukilinganisha na Android na ChromeOS ambazo karibu asilimia 90 zinaendana.
Kama Google wakifanikiwa kuunga programu-endeshaji zake mbili, watakuwa mbioni kufanya kile ambacho Microsoft wanajaribu kufanya na mpango wao wa Continuum unaoanza kuonekana kwenye Windows 10 kwa vitumi vyote. Kampuni nyingine inayotazamia kuwapa watumiaji wake hisia moja ya utumiaji kwa vitumi vyote ni Canonical inayotengeneza programu-endeshaji ya Ubuntu.
Chanzo: Fortune.com
2 Comments