Kampuni ya Zipline kushirikiana na serikali ya Tanzania wataanza kurusha ndege zisizo na rubani kwaajiri ya kusambaza madawa katika hospitali zilizo maeneo ya vijijini.
Tayari kampuni hii imekwisha fanikiwa sana nchini Rwanda ambako tangu mpaka mwezi Mei walikwisha fanya safari 350 za mafanikio.

Je hii teknolojia ya kusambaza dawa kwa kutumia ndege isiyo na rubani inafanyaje kazi?
Kwa maneno mepesi ni kwamba kampuni hii inatumia Ndege zisizo na rubani (ambazo zinajulikana kama Drones) kupeleka mzigo (huu unaweza damu salama, dawa ama kifaa kwaajiri ya tiba), ndege hizi huruka kwa mwendo wa zaidi ya kilomita mia kwa saa na pindi zinapofika katika kituo cha afya ama hospitali huangusha mzigo ambao huangushwa na parashuti.
Drone hizi zinazozungumziwa hapa ni za aina gani?
Najua tayari umekwishaona Drone (ndege zisizo na rubani) katika upigaji picha (harusini ama katika matukio mengine) tayari ndege zisizo na marubani zinatumika lakini ndege ambazo Zipline wanatumia ni tofauti kidogo, kampuni hii inatuma Drone ambazo zinamundo kama ndege ya kawaida ila ni ndogo ukilinganisha na ndege za kawaida pia zinakwenda katika mwendokasi mkubwa kushinda drone za matumizi ya kupiga picha.

Drone hizi zinasifa zipi?!
Zipline inatengeneza drone ambazo zina mabawa yenye urefu wa futi 6, ndege hii inauwezo wa kukimbia hadi kilomita 110 kwa saa. Ndege hizi zitaweza kubeba uzito wa takribani kilo 1.4, dawa ama damu salama na mizigo mingine ambayo ndege hii inabeba haizidi uzito huu.
Ndege hizi zinatumia umeme badala ya mafuta, kila ndege inabetri ambayo inachajiwa kabla ya kuanza safari. Betri ya ndege hii inao uwezo wa kusafire safari ya hadi kilomita 160 na zaidi kabla ya kuhitaji kuchajiwa tena.

Ndege hizi zinatumia GPS na mitandao ya simu kwaajiri ya kufikia vituo vya afya, pamoja na hilo ndege hizi ambazo zimepewa jina la Zips zinao uwezo wa kufanya kazi usiku na mchana katika mvua na jua na hata upepo mkali.
Ndege hizi hurushwa kutoka katika kifaa maalumu na husafiri mpaka kituo husika kisha hudondosha mzigo na kurudi katika kituo cha usambazaji ambako ndege hii hutua katika puto bila uharibifu tayari kwaajiri ya kutumwa tena.
Hii ni habari njema kwa Tanzania ambayo pamoja na mambo mengi imekuwa ikijitahidi kufikisha huduma za afya kwa watu wengi zaidi, Endelea kufuatilia mtandao wa Teknokona kwa taarifa mbalimbali za teknolojia katika lugha yako adhimu ya kiswahili.