Simu janja zipo za aina nyingi sana siku hizi na zinakuja katika ukubwa na maumbile tofauti tofauti hata Os zake ni za utofauti. Lakini ni mambo gani sasa utakayoifanyia simu yako ili kuifurahia zaidi?
Kwa watu wengi wakinunua simu kwa mara ya kwanza kabisa kitu cha kwanza wanachofikiriaga huwa ni kava lakini kumbuka hii ni karne ya 21 na kuna mambo mengi yanayohitajika katika simu janja zetu ukiachana na makava.
Vitu Vya Kuwa Navyo Ni:
1. Betri La Nje (Power Bank)
Kama hutaki simu yako ikuishie chaji wakati ukiwa katika hali ya kuwa unaihitaji basi huna budi kuwa na Betri la nje (Maarufu sana kama Power Bank). Najua fika kwa maisha yetu ya kitanzania na masimu yetu makubwa makubwa yanayoongoza kumaliza chaji ya simu basi ni muhimu kuwa nayo.
Chaja za nje zipo zenye uwezo tofauti tofauti ambao unazitofautisha hata katika bei. Kama una safari ndefu basi chaja zenye 10,000 mAh au 20,000 mAh zinaweza zikawa ni msaada mkubwa katika safari yako.
2. HeadPhones/Earphones
Ndio mara nyingi tunazitumia katika kusikiliza muziki, kuangalia video au hata kuongelea wakati ukipigiwa. ‘Earphone’ au ‘Headphone’ ni msaada mzuri sana hasa ukiwa maeneo ambayo huwezi ukashika simu, unaweza ukazifaa na ukaendela kuongea na mtu katika simu.
3. Kilindio Cha Skrini Ya Simu Janja (Screen Protector)
Simu ambayo haina hii kitu kioo chake kipo katika hati hati ya kuchakaa ndani ya muda mfupi. Hasa simu zetu za kugusa na kidole ndio zinakuwa matatani hasa pale zinapokuwa hazina ‘Screen Protector’ . Protector zipo za aina nyingi sana kuanzia za nailoni mpaka za glasi na zina msaada mkubwa hata katika kuzuia simu janja zetu kuvunjika kioo pale zinapoanguka.
4. Kava Gumu La Nje Ya Simu
Ukiwa na kava gumu unakuwa na hali Fulani hivi ya kujiamini pale simu janja yako inapoanguka chini, Ndio! nah ii ni kwasababu makava hayo magumu yanasaidia sana katika kuilinda simu isipate majeraha ya nje.
Mara nyingine makava haya ya simu yetu hutuongezea vitu vidogo vidogo ambavyo tunavitumia kwa mambo mengine kama vile Wallet na Sehemu ya kuwekea kadi zako muhimu.
5. Chaja (USB na Kichwa Cha Ukutani)
Kulingana na hayo yote yaliyosemwa chaja ni kitu muhimu sana cha kuwa nacho na hasa ile yenye waya wa USB na kichwa cha ukutani (vikiwa vimetenganishwa). Ukiwa na hivi hata kama simu yako imezima kwakukosa chaji basi ukipata eneo tuu ambalo unaweza ukachaji – kwa mfano kwenye migahawa – utaweza kupata msaada hata wa kubusti (kuchaji kidogo) simu janja yako.