Toleo jipya kabisa la programu endeshaji ya Android la Android 6, Marshmallow linatumika kwenye asilimia 2.3 tuu ya vifaa vinavyotumia Android – simu, tableti n.k. Hii ikiwa ni takribani miezi 5 tokeo toleo hilo lianze kupatikana rasmi.
Katika data zilizowekwa wazi na Google pia zinaonesha toleo la Android Lollipop kuwa ndilo linalotumika zaidi, hii ikiwa ni kwa asilimia 36.1.
Ingawa toleo la Android Marshmallow linaonekana utumiaji wake bado ni mdogo hali inaweza kubadilika hivi karibuni.
Tayari simu nyingi mpya zinakuja na toleo hili, na pia tayari watengenezaji simu wakubwa kama Samsung na wengine tayari wapo kwenye harakati ya kusasisha (update) baadhi ya simu zao za kisasa zilizouzika zikiwa na matoleo ya Android yaliyopita ndani hichi kipindi cha miezi michache.
Toleo la Android 6.0 ( Android Marshmallow) lina miezi mitano tuu tokea lianze kupatikana… Katika pindi cha miezi yake mitano ya mwanzo toleo la Lollipop lilifanikiwa kufikisha utumiaji wa asilimia 5.4.
Kwa undani – Matoleo ya Android yanayotumika kwa sasa duniani kote
- Marshmallow – 2.3%
- Lollipop – 36.1%
- KitKat – 34.3%
- Jelly Bean – 22.3%
- Ice Cream Sandwich – 2.3%
- Gingerbread – 2.6%
Hali hii ya ucheleweshwaji wa watumiaji wengi kupata masasisho ya toleo la Android la kisasa zaidi kwenye simu zao huwa linasababisha kitu kinachofamika kama ‘fragmentation‘.
Hii ni kwamba watengenezaji apps wanapata kazi kubwa ya zaidi kutengeneza apps zinazoweza tumika katika matoleo hayo tofauti ya Android, hasa pale ambapo kuna utofauti mkubwa umefanyika kati ya matoleo ya Android husika. Hii ni tofauti ukilinganisha na programu endeshaji ya iOS inayotumika kwenye iPhone na iPads, kwani kwa data za mwezi wa kwanza zilionesha asimilia 75 ya watumiaji wake tayari wanatumia toleo jipya kabisa la iOS 9. Inategemewa ujio wa simu mpya za kisasa zaidi kwa mwaka huu kama Samsung Galaxy S7 n.k zitasaidia kukuza asilimia ya watumiaji wa Android Marshmallow pia.
Je unatumia simu yenye toleo gani la Android? Na huwa unaangalia toleo la Android kabla ya kununua simu?
Vyanzo: AndroidDevelopers na mitandao mbalimbali
One Comment
Comments are closed.