Samsung wapo njiani kuja na teknolojia ya mabetri ya simu yanayodumu zaidi na chaji kutokana na utumiaji wa malighafi mpya katika utengenezaji.
Madini aina ya ‘graphene’ yatatumika kama malighafu katika utengenezaji wa mabetri ya aina ya lithium yanayotumika kwa sasa kwenye simu.
Teknolojia hiyo mpya waliokuja nayo inafanya betri la simu liweze kudumu muda mrefu kwa matumizi mengi baada ya kuchaji ukilinganisha na ubora wa mabetri yanayotengenezwa kwa teknolojia inayotumika sasa hivi.

Samsung walitambulisha rasmi ugunduzi wa teknolojia yao mwaka 2004 ila hadi sasa walikuwa katika utafiti zaidi katika kuhakikisha ubora, usalama na uwezo wa kutengeneza mabetri hayo.
- Faida iliyoonekana kutokana na teknolojia hiyo;
- Mabetri kuwa na ujazo cha chaji mkubwa zaidi
- Kuweza kuchajiwa kwa haraka zaidi
- Pia yanaweza kuhimili mahitaji makubwa ya chaji kwa wakati mmoja
– vyote hivi vinafanikiwa bila betri hilo kupata joto haraka.

Hadi sasa changamoto wanayopambana nayo ni kupunguza gharama zinazotumika katika uzalishaji wa betri hizi. Kwa wastani imeonekana teknolojia hiyo ina wastani wa gharama kubwa kwa kila utengenezaji wa betri moja ukilinganisha na mabetri yanayotumika kwa sasa.
Hili tunategemea litashuka baadae, ni kawaida gharama za bidhaa au teknolojia mpya kuwa juu sana kutokana na kutokuwa na mfumo mzuri wa upatikanaji wa malighafi na pia vifaa vya teknolojia vya utengenezaji wa bidhaa kwa wingi na kwa upesi.