Tanzania, tuko mbioni kuingia kwenye orodha ya mataifa yenye sheria kali sana za utumiaji wa mtandao. Kwa kizungu wanaziita ‘draconian’ laws.
Muswada wa sheria hiyo umeangalia makosa kama vile kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na pia kusambaza picha za utupu za watoto.
Je nini ufahamu kwa sasa;
-Ukikutwa na kosa la kusambaza picha za ngono, uasherati na matusi basi utakuwa njiani kupigwa faini ya Sh milioni 30 au kwenda jela miaka 10! Upo apo?
-Pia ukikutwa na kosa la kusambaza picha za utupu, yaani uchi, basi utalipa faini isiyopungua milioni 29 au kwenda jela miaka 7.
-Pia kama mtu atatoa taarifa, takwimu au maelezo kwa njia ya picha au maandishi au aina nyingine zozote zikiwa ni za uongo, akipatikana na hatia basi atatakiwa kulipa faini isiyopungua Sh. milioni 3 au kwenda kifungoni miezi sita (HII NI MOJA YA SEHEMU INAYOTISHA SANA, KWANI VYANZO VYA TAARIFA AU TAKWIMU NI VINGI NA MTU ANAWEZA AKASAMBAZA TAARIFA AMBAYO INAMAKOSA BILA KUGUNDUA)
Baadhi ya vifungu:
Taarifa za uongo;
16. Mtu yeyote anayetoa taarifa, data au maelezo kwa njia ya picha, uongo maandishi, alama au aina nyingine yoyote kwenye mfumo wa kompyuta, endapo taarifa, data, au maelezo hayo ni ya uongo, yanapotosha au yasiyo sahihi, atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia adhabu ya kifungo kisichopungua miezi sita au vyote.
Uonevu na unyanyasaji
23.-(1) Mtu hataanzisha au kukadimisha mawasiliano yoyote ya kielektroniki kwenda kwa mtu yoyote kwa kutumia mfumo wa kompyuta, kwa lengo la kurubuni, kulazimisha, kutisha au kunyanyasa au kusababisha maudhi ya hisia. (2) Mtu akataye kiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na atawajibika, iwapo atatiwa hatiani, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia kifungo kwa kipindi cha kisichopungua mwaka mmoja au vyote.
Jambo zuri ni kwamba ni kweli tumefikia sehemu tunaitaji muswada wa kudhibiti masuala ya kimtandao, ila kwa kiasi kikubwa kuna uonekano mchakato huu umepelekwa kwa kasi sana na ingebidi wadau mbalimbali tungepewa muda zaidi wa kuboresha mapungufu yake mbalimbali.
Moja ya jambo baya zaidi ambalo ata wabunge wa upinzani waliliongelea sana jana ni nguvu walizopewa polisi katika taratibu zote za ukamataji wa watu pamoja na vifaa au data husika. Kwa mfano kama polisi wanawasi wasi na wewe basi wataweza kukushika na kwa ruhusu ya mkuu wa kituo itabidi uwasilishe vifaa vyako hii ikiwa ni pamoja na ‘password’ ili waweze kufungua/kutazama data hizo. Suala hili ili kuwalinda wananchi na data muhimu za kibinafsi ya faragha ingekuwa ni jambo zuri polisi kuweza kufanya hivi kwa ruhusu ya mahakama tuu na si vinginevyo kama ilivyowekwa sasa.
Tulishawahi kuomba mtazamo wa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu masuala ya Cyber Crime pamoja na mambo ya usalama wa huduma kama za ‘Simu Benki’, akatuhaidi kufanya hivyo ila baadae mawasiliano yetu yakaachwa kujibiwa. Ila bado tunaamini kuna umuhimu sana wa mswada huu kufanyiwa maboresho muhimu hasa kwa ajili ya kutulinda wananchi kutoka kwenye kesi za kubambikiziwa n.k. Kuja kwa sheria hii ni jambo zuri ila kuja na kupitishwa kwa haraka haraka bila ushirikishwaji wa wadau wengi zaidi si jambo zuri. Kwa sasa wa kutuokoa katika hili ni Rais tuu.
TeknoKona tunaungana na wengine wote katika kumsihi Mheshimiwa Rais kutopitisha mswada huu kuwa sheria, haurudishe ufanyiwe maboresho mazuri taratibu hii ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wadau wengi zaidi.
Kuusoma Mswada wote kwa lugha ya kingereza bofya hapa; -> CYBERCRIMES-ACT-2015(PDF)
Soma tamko la baadhi ya wadau hapa chini, hapa pia ubovu wa muswada huu umeelezewa vizuri tuu;
TAMKO LA WADAU NA WATUMIAJI WA MITANDAO YA KIJAMII NCHI TANZANIA.
31/03/2015
Ndugu Waandishi wa habari, Tunapenda kutanguliza shukrani za dhati kwenu kwa kufika katika eneo hili kutusikiliza.Mbele yenu ni wawakilishi wa wa wadau mitandao ya kijamii nchini Tanzania.Ndugu waandishi wa habari,si kawaida na wala mazoea kwa wadau na watumiaji wa mitando ya kijamii nchini kukutana kwa pamoja ama kwa uwakili kuzungumza na nyie wanahabari kama inavyotokea hii leo.
Ndugu wanahabari, vikao vya bunge la Jamhuri vinavyoendelea mjini Dodoma vimepokea miswada kadhaa ya serikali inayotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hilo na kisha rais kuridhia kwakusaini na kuwa sheria rasmi.
Ndugu wanahabari, baadhi ya miswada hiyo iliyowasilishwa ni pamoja na Mswada wa Mahakama ya Kadhi, Mswada wa ongezeko la kodi la 100%, Mswada wa Sheria ya habari na uhalifu wa kimtandao na mingine mingi. Hii ni hatua mhimu na nzuri katika ukuaji wa taifa kiuchumi na kijamii hasa kama dhamira ya miswada hii itakuwa na maslahi kwa taifa na sio maslahi ya kisiasa.
Ndugu wanahabari, tumewaiteni hapa ili kuzungumzia mswada wa habari na uhalifu wa kimtandao, tumefanya hivyo kutokana na unyeti wa swala hili na aina ya mswada uliofikishwa Bungeni na NJIA iliyofuatwa ili kuufikisha Bungeni mswada huo, Tunaipongeza serikali kwaDHANA ya mswada huu lakini tuna LAANI mantiki ya mswada huu na njia ulizopita mpaka kufika Bungeni.
Ndugu zangu wanahabari, tambueni kuwa hakuna uhuru usio na mipaka na tambueni kuwa uhuru wenye mipaka ni UTUMWA, Mitandao ya kijamii imekuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi na kifikra, vile imeleta uhalifu mpya na wenye kuleta changamoto kubwa katika dunia ya tatu, hivyo uwepo wa sheria nzuri na zenye mantiki katika taifa lolote ni uhai na afya kwa taifa hilo, lakini sheria hizo ni vema zikawahusisha wadau halisi wa mitandao ya kijamii kuliko serikali za mataifa kuunda sheria hizo na pengine serikali hizo hazijua hata maana ya uhalifu wa kimtandao na mtandao wenyewe. Na kibaya zaidi mswada huu umepelekwa Bungeni kwa HATI ya DHARULA, ipi mantiki ya kupeleka kwa hati ya dharula?
Ndugu wanahabari,sisi kama vijana na wadau mhimu wa mitandao nchini. TUNAPINGA kwa nguvu zote mswada huu kutokana na mapungufu makubwa ya kimantiki, Mapungufu makubwa ya kimantiki ya mswada huu ambayo kimsingi yameufanya mswada huu wenyewe uwe ni UHALIFU dhidi ya ubinadamu yanaainishwa katika vifungu vifuatavyo hapa chini, ambapo kila mdau ni lazima aone.
Kwa ufupi, serikali imeamua kupoka uhuru wa kifikra wa watu na kuwaamlia upi ukweli na upi uongo. Huu ni ubakaji mkubwa wa Demokrasia haki ya kikatiba
SEHEMU YA VIFUNGU VYENYE UTATA NA HATARI ZAIDI KWA UMMA.
“Kutoa taarifa za Uongo”
16.- Mtu yeyote anayetoa taarifa, data au maelezo kwa njia ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote taarifa, data, kwenye m fumo wa kompyuta, endapo au maelezo hayo ni ya uongo, yanapotosha au yasiyo sahihi, atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia adhabu ya kifungo kisichopungua miezi sita au vyote.
Na pia, kipengele cha 21 katika mswada huo kinahusu watoa huduma.
21.-(1) Mtoa huduma anayepokea amri kuhusiana na upelelezi wa kijinai, inayohitaji usiri, hatatoa taarifa yoyote iliyopo kwenye amri hiyo isivyo halali na makusudi.
(2) Mtu akatayekiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na atawajibika, iwapo atatiwa hatiani, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu au vyote.
Aidha, serikali hii tukufu imeamua kutumia kifungu cha 22 kuonyesha dhamira yake si ya kutania endapo itataka kupata taarifa za mtu na mtoa huduma akataka kuua ushahidi kama inayosomeka:
22. Mtu ambaye kwa makusudi na kinyume cha sheria ataharibu, atafuta, ataondoa, ataficha, atabadilisha au ataifanya data kompyuta kukosa maana kwa lengo la kuharibu ushahidi au kuchelewesha upelelezi atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini ya kiwango kisichopungua milioni tatu au kutumikia kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja au vyote.
(2) Mtu ambaye kwa makusudi atazuia utekeleza au atashindwa kutekeleza amri iliyotolewa na sheria hii, atakuwa ametenda kosa na atawajibika, iwapo atatiwa hatiani, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia kifungo kwa kipindi cha kisichopungua mwaka mmoja au vyote.
“Utoaji Data Kwa wachunguzi”
32.-(1) Pale ambapo data inanitajika kuwekwa wazi kwa madhumuni ya uchunguzi wa kijinai au kuendeshwa kwa kesi mahakamani, Askari Polisi Mkuu wa kituo au afisa mtekelezaji wa sheria mwenye cheo cha askari mkuu wa kituo anaweza kutoa amri kumtaka-
(a) mtu yeyote kuwasilisha data iliyoainishwa ambayo mtu huyo anaimiliki au iliyo chini ya uangalizi wake ambayo imehifadhaiwa kwenye mfumo wa kompyuta; au
(b) mtoa huduma yeyote, kuwasilisha taarifa kuhusiana na mteja zilizo kwenye umiliki au uangalizi wake.
(2) Iwapo kitu chochote kinachohusiana na upelelezi kinajumuisha data iliyohifadhiwa kwenye mfumo wa kompyuta au kwenye kifaa, amri itachukuliwa kumtaka mtu kutoa au kuruhusu upatikanaji wa data hiyo katika namna ambayo inasomeka na inayoweza kuondolewa.
Ndugu wanahabari,Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Sehemu ya TATU,
Haki ya Uhuru wa Mawazo Uhuru wa Maoni.
Sheria ya 1984 Na.15 ib.6 18.- inasema hivi,
(1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yakekutoingiliwa kati.
(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Ndugu zangu wanahabari tunapenda kuishauri serikali hii kuondoa hati ya dharula ya mswada huu ili ujadiliwe kwa mapana yote na kupata sheria nzuri inayolinda utu na uhuru wa watu wake. Kinyume na hapo tunatamka kama ifuatavyo,
Sisi wadau tunaiambia serikali hii sikivu kuwa kuandaa mswada wa sheria bila kuwashirikisha wadau wa sekta hiyo ni kutangaza vita dhidi yao, nasi tutajibu mwito huu bila choyo. Tunaiambia serikali hii sikivu kwamba masaa 24 kuanzia sasa tutaendesha kampeni ya kuhakikisha mswada huu haupitishwi kwa njia ya sheria na taratibu za kibunge labda iwe kiuhalifu hivi hivi kama ulivyopelekwa bungeni.. Hatupendi na hatupo tayari kuizuia serikali hii kuendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao lakini tukilazimishwa kufanya hivyo tutafanya.
Sisi wadau wa mitandao ya kijamii tunatamka kwamba tutaendesha kampeni kwa nguvu zote kuhakikisha watu hawapigi kura ya maoni ya katiba pendekezwa ya ccm.
Nazaidi tutaenda mbali kuhakikisha wananchi wote hawaichagui tena ccm uchaguzi wa mwezi wa kumi.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki teknohama
Asante sana kwakunisikiliza
YERICKO NYERERE
Mratibu wadau wa mitandao ya Kijamii
No Comment! Be the first one.