Tangia simu ya kwanza ya iPhone kutoka kampuni la Apple kutoka mwaka 2007, simu kwa ujumla zilibadilika. Zilibadilika kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye kuwa simu tuu mpaka kuwa simu janja. Sasa hivi simu yako unaweza fanya nayo mambo mengi sana ambayo hata hukuweza fikiria
Hivi ulishawahi fikiria kuwa simu zetu hazitakuwa na kazi ya kupiga na kupokea simu pengine na kutuma meseji tuu? Simu janja zimebadilisha maisha yetu yetu kwa ujumla kwa kiasi kikubwa tuu. Kuna wengine siku hizi wanadiliki mpaka kusema kuwa hawawezi kuishi bila simu zao.
Nisiongee sana ngoja nikujuze vitu hivyo ambavyo Simu janja zetu imeviwezesha
-
Tochi
Kwa hii ilikua ni kitu cha kawaida kwa simu za kichina lakini sasa mpaka simu janja zinakuja zikiwa na kipengele hiki. Pia hata kama simu janja yako haina kipengele hiki una uwezo wa kushusha (download) tochi katika soko la simu yako. Sasa haina haja ya kutembea na matochi makubwa, simu yako tuu inatosha
-
Saa, Kengele
Wengi kwa sasa wanaovaa saa ni kwa ajili ya mapambo, wengi wanatazama simu zao kujua muda. Hata makampuni sasa yanajitahidi kutengeneza saa ambazo ni sawa na kompyuta ndogo tuu kwa mfano tazama iWatch. Simu janja zetu sio tunazitumia tuu kwa kuangalia saa bali hata katika kuseti kengele (alarm).
-
Ramani, Vifaa Vya GPS
Hapo zamani hata ramani ya kasehemu kwa mfano pale posta, ilibidi utoe kwenye fotokopi ili utembee nayo ikuelekeze. Simu janja ndio kila kitu, vitu kama ramani tulikua tukiangalia katika Atlasi lakini sasa vyote ndani ya simu. Kwa sasa ukiwa unatumia Atlasi labda wakati unacheza kale kamchezo ka kutafuta nchi (Hah!!). Apps kama Google Maps na Nokia Maps inafanya kazi zote katika kuhakikisha unapata ramani bomba kabisa za duniani kote. Bado katika App hizo unapata huduma ya GPS, kwa mfano unaweza ukanganisha simu mbili na kujua moja iko wapi kwa kutumia nyingine.
-
Vinasa Sauti
Sasa hata waandishi wa habari naona wanatumia simu janja zao kukusanya taarifa mbalimbali kwa kunasa sauti. Sawa sikatai kama unafanya kazi za kitaaluma flani ambazo zinakubana utumie vinasa sauti kama vile maiki ni sawa tuu. Lakini kama unataka tuu kunasa sauti za ubora wa kawaida tuu huna budi kutumia simu janja yako tuu kwa utapata taarifa hiyo kwa kiwango kizuri kwa njia ya sauti.
-
Kioo
Ulishawahi fikiria simu janja yako unaweza kuwa kama kioo. Haya sasa kama una simu janja yenye kamera ya mbele, ile kamera yako inaweza tumika kama kioo. Kwa hili madada wengi watakuwa wananielewa kwa sana. Kamera ya simu janja yako ile ya mbele unaweza itumia kama kioo na kuweka mambo yako sawa kwa mfano kama kuangalia jinsi Tai yako ulivyo kaa n.k
-
Malipo
Simu janja zetu sasa zinafanya malipo. Hivi sasa unaweza agiza chakula kutumia simu janja yako na kikija unalipa kwa kutumia simu janja yako. Hakuna haja ya kwenda benki kwa upande mwingine Mpesa, TigoPesa, EasyPesa, AirtelMoney na VMoney (halotel) zipo kwa ajili ya kukamilisha miamala mbali mbali kutumia simu yako. Pia kuna Benki za kimtandao kama vile Paypal ambazo unaweza tumia miamala, katika simu janja yako unaweza kuwa na App zake ili kukurahishia kazi zote hizo za kibenki.
-
Kamera, Kamera Za Video
Muda unavyozidi kwenda matumizi ya kamera za kawaida yanapungua kwani simu janja siku hizi zinapiga na kutoa picha katika kiwango cha juu sana. Licha ya picha simu janja siku hizi zina uwezo wa kurekodi video katika kiwango cha juu (4K). Simu za iPhone zile za iPhone 6s na iPhone 6s plus zina uwezo mkubwa wa kurekodi video na pia zinatumika katika baadhi ya makampuni makubwa katika kurekodi video za hali ya juu tuu.
-
iPod, Radio
Kama muziki na redio unavipata katika simu janja yako kuna haja gani ya kuwa na vitu hivyo? Nakumbuka zamani kipindi cha mpira utawakuta wazee na viredio vyao wakiwa wameviweka karibia na masikio kama vile vinawaambia siri. Vile vile iPod watu hawana mpango nazo siku hizi. Kumbuka hata mauzo ya iPod katika kampuni la Apple yalishuka kwani kila kitu ambacho watumiaji walikipata katika iPod kipo katika iPhone na zaidi. Watumiaji wengi wa iPod wakaona ni bora wawe na simu janja ambayo wanaweza jaza miziki. Simu janja siku hizi zinakuja na redio au hata kama hazijaja nazo una uwezo wa kusikiliza redio hizo katika mtandao au hata kuzishusha
-
Kupunguza Ada Ya Kutuma Meseji/Ujumbe Na Kupiga Simu Mbali
Siku hizi mtu alie mbali kabisa unaweza wasiliana naye kwa kutumia gharama ndogo kwa sababu ya simu janja zetu. Tofauti na zamani ambapo watu walikuwa hawaongea na hata wakiongea wanatumia mda mchache sana. App kama WhatsApp na Skype zinatuwezesha kuwasiliana na watu waliopo mahali popote duniani kwa urahisi ili mradi tuu uwe na bando la kutosha.
-
Kuondoa Wazo La Simu Kama Kifaa Kimoja
Kwa sasa teknolojia imekua kwa kiasi kikubwa sana hivyo sasa kama nilivyoeleza hapo mwanzo simu sio kifaa kimoja kama mwanzo cha kupiga, kupokea simu na kutuma meseji. Simu janja zinaweza tumika kama vifaa vingine lukuki.kadri muda unavyozidi kwenda simu hizi zinakuwa sio simu tena bali ni kompyuta.
Tuzishukuru simu hizi pia kwani tunaingia katika mitandao ya kijamii na kukamilisha mengi kwa kutumia simu janja zetu. Mengi tunaweza fanya siku hizi kwa kutumia simu zetu janja. Kila kampuni la kutengeneza simu linapambana kuhakikisha linaleta simu iliyo janja zaidi sokoni. Yapo maajabu mengi ambayo simu janja zimewezesha lakini hayo niyale macheche tuu tuliyokuandalia kwa wakati huu
No Comment! Be the first one.