Suala la kumpatia mtu mwingine password (kwa kiswahili – nywila) ni moja ya jambo ambalo wengi huwa hawaliamini. Watakuuliza kwa nini nifanye hivyo?
Kabla ya kwenda mbali ningekukumbusha hapo juu kwenye kichwa cha habari tumetumia ‘Mtu wa Karibu’, hivyo hapa tunamaanisha mtu unayemuamini, na si mtu yeyote tuu.
Katika kuliangalia hili ningependa kuanza na sababu za mbili za msingi au mazingira yanasababisha kufanya jambo hilo lionekane ni jambo la lazima au muhimu kufanya.
- Kuna kifo, je ukifa unataka kuacha akaunti iwe kama ilivyo? Vijukuu vyako na vilembwe vije kuona ulichoandika siku moja ukiwa umelewa balaa?
- Kuna kusahau password. Ndio kabisa, hasa kwa watu wazima wanaoelekea uzeeni au mtu mwenye ugonjwa unaoweza sababisha hali ya kusahau. Kwa hili ni vizuri kama utakuwa na mtu au sehemu inayofikika haraka uliyohifadhi password hizo.
Ni nani hasa unaweza mpatia taarifa za password yako?
Ni vigumu kukushauri umpatie nani hasa, wakati wengine huwa wanapeana na wapenzi wao wengine huwapaga marafiki zao wa karibu. Wakati watu wengine wanaona kwa wapenzi kufahamu password za mwingine ni jambo kwenye uhusiano wao pia zipo tafiti zinazosema ni kitu cha hatari na kina weza kuwasababishia ugomvi usiokuwa wa lazima.
Njia nyingine ambayo wengi wanaitumia katika nchi zilizoendelea ni kuziandika password zako zote kwenye karatasi/daftari linalokaa sehemu ya karibu. Hii itakusaidia ata wewe mwenyewe pale unaposahau password husika au pale utakapokuwa umefariki n.k – ili mtu wako wa karibu aweze kufunga akaunti hizo au kuitengeneza vizuri akiacha mambo muhimu ya kihistoria katika maisha yako yabakie huku akiondoa vingine vyote visivyokuwa na ulazima.
Je kwa mtazamo wako ni vizuri mtu mwingine kujua password za mitandao yako ya kijamii na barua pepe ili aweze kukusaidia baadae? Unamaoni gani juu ya suala hili? Sababu gani nyingine unadhani ni ya muhimu sana kufanya wewe umpatie mtu mwingine password yako?
One Comment