Makampuni mengi ambayo yanajishughulisha na utengenezaji wa simu janja yanatoa bidhaa mpya kila baada ya muda fulani na wakati mwingine hata kwa mkupuo. Siku ya leo rununu Redmi 7 imewekwa wazi na ni simu nzuri ambayo ina bei ya kawaida.
Wakati unafikiria kununua simu kuna mambo ambayo unaweza ukawa umevutiwa nayo kwenye hiyo ambayo unapanga kuinunua na kama ni mtu ambae unajua sifa za rununu nzuri bila shaka utakuwa ukifurahia uamuzi wa kuhama kutumia simu moja hadi nyingine. Redmi 7 nimeiweka kwenye kundi la simu nzuri kutokana kipuri mama, uwezo wa betri, RAM kuwa vizuri. Sasa tuangalie kipengele kimoja baada ya kingine kwa undani:
Kipuri mama/Ubora wa kioo
Redmi 7 imewekwa Snapdragon 632 (vipuri 8 ndani ya simu moja vikiwa na kasi ya 1.8GHz) kitu ambacho kinasaidia simu kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu. Upande wa urefu wa kioo kina inchi 6.26 ubora wa LCD+HD (1520 x 720 pixels).
Kamera+Betri
Kwa hapa simu husika imewekwa kamera zenye uwezo unaoridhisha ingawa si wa hali ya juu nikimaanisha kamera za nyuma zipo mbili (2); moja ina MP 12 na nyingine MP 2. Kamera ya mbele ina MP 8. Kwenye upande wa betri inaridhisha sana kutokana kuwa na nguvu lakini imekwenda mbali zaidi na kuwa na teknolojia ya kuchaji haraka; bertri lake lina 4000mAh, 10W kwa ajili ya kuruhusu mfumo wa kuchaji haraka.
RAM/Diski uhifadhi+Bei
Redmi 7 hapa imewekwa uwezo tofauti tofauti kuanzia yenye uwezo mdogo hadi mkubwa- 2/16 GB, 3/32 GB na 4/64 GB. Bei ya simu husika ni kuanzia $105|Tsh. 241,500, $120|Tsh. 276,000 na $150|Tsh. 345,000.
Programu endeshi+Sifa nyinginezo
Redmi 7 imewekwa Android 9 Pie huku ikwa na teknolojia ya kuzuia maji, AI, ulinzi wa kidole, USB Type C, rangi ni Bluu, Nyekundu, Nyeusi.
Redmi 7 ndio hiyo na wewe ndio wa kufanya maamuzi ya kuinunua au la! pale itakapoingia sokoni Machi 26. Vipi wewe msomaji wetu unaizungumziaje simu husika? Ni ya bei ya kawaida?
Vyanzo: India Today, GSMArena