Kabla ya kufahamu kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya wadukuzi mtandaoni ni vyema tungejua kwanza kuwa mdukuzi ni nani ?. Mdukuzi ni mtu anayetumia ujuzi wake wa tehama na mtandao kuiba taarifa za mtu binafsi au kuingia kwenye mfumo bila ruhusa.
Ukuaji wa teknolojia umepelekea kurahisishwa kwa mawasiliano pamoja na kuongeza matumizi ya mtandao. Hali hii imepelekea kuwepo kwa mianya inayowaruhusu wadukuzi kuiba taarifa za watu au kusababisha hitilafu katika mifumo ya kampuni na mashirika mbalimbali.
Taarifa zinazolengwa na wadukuzi wanapofanya uvamizi ni taarifa za mtu binafsi ikiwemo majina yako kamili, baruapepe yako, tarehe ya kuzaliwa, kazi na anuani yako. Wadukuzi hulenga pia taarifa za matumizi yako ya mtandao, baruapepe yako, akaunti zako za mitandao ya kijamii na taarifa zingine nyingi. Mdukuzi anapokuwa na taarifa hizi anaweza kuiba hela zilizopo kwenye kadi yako ya benki unayotumiaga kufanya malipo mtandaoni, anaweza kuiba utambulisho wako na kufanya uhalifu halafu ukawajibishwa wewe.
Chukua hatua zifuatazo kujilinda dhidi ya wadukuzi mtandaoni
Usifanye muamala wowote mtandaoni kwa kutumia Wi-fi ya bure: Kwa kufanya hivi unakuwa umepunguza uwezekano wa mdukuzi kunasa taarifa zako za miamala ya fedha kama namba ya siri, akaunti namba na jina la akaunti.
Zima programu zote zinazotumia mtandao ambazo hauzitumii mara kwa mara: Kuna baadhi ya programu zinatumia mtandao lakini wewe binafsi hauzitumii muda wote, Hakikisha kila baada ya kumaliza kuzitumia unazizima ili zisiendelee kuchota taarifa mtandaoni. Hii itakusaidia kugundua mabadiliko madogo madogo ya matumizi yako ya mtandao yatakayopelekea wewe kugundua mapema kama umedukuliwa au kama unadukuliwa muda huo.
Pakua programu katika sehemu au tovuti halali: Unapopakua applikesheni katika tovuti zisizo za halali unawatengenezea wadukuzi mianya ya kupita na kufanya udukuzi katika kifaa chako kwasababu unakuwa unatumia applikesheni isiyo salama.
Kuwa makini na tovuti pamoja na viambatanisho unavyofungua: Mashambulizi mengi ya wadukuzi hupitia kwenye baruapepe, wanapendaga kutumia njia hii ili kukusanya taarifa zaidi kabla ya kufanya shambulizi lenyewe hivyo kuwa makini na usiingie kwenye tovuti utakayotumiwa kwenye baruapepe usiofahamu mtumaji. Pia usifungue viambatanishi vya kwenye baruapepe kama haujamjua aliyekutumia ni nani na nini kipo kwenye kiambatanishi hicho.
Tumia programu za kujilinda dhidi ya virusi: Kuna progamu mbalimbali maalum kwaajili ya kuzuia virusi vya kwenye simu au kompyuta pamoja na kusimamia matumizi yako ya mtandao. Programu hizi zinaongeza ukuta wa usalama katika kifaa chako na hivyo kuwapa ugumu wadukuzi kuiba taarifa zako.
Tumia nywila kufunga kifaa chako: Hakikisha unatumia nywila imara yenye herufi kubwa na ndogo, namba pamoja na alama mbalimbali za uandishi kama reli (#) katika kifaa chako. Kwa kufanya hivi utakuwa umewaongezea ugumu wadukuzi kuotea nywila yako.
Futa taarifa za matumizi yako ya mtandao: Unapozifuta taarifa za matumizi yako ya mtandao unawaondolea wepesi wadukuzi kujua namna ya kukuvizia unapokuwa mtandaoni kwani watashindwa kufahamu ni tovuti zipi unapendelea kuzitembelea.
Endelea kutembelea tovuti yetu kufahamu zaidi kuhusu matumizi salama ya mtandao. Pia unaweza kusoma makala zetu zingine hapa.
No Comment! Be the first one.