Kwa muda wa wiki sasa kuna habari zinazoenea ya kwamba kampuni ya Apple inaweza ikawa inataka kutengeneza gari. Je kuna ukweli wowote?
Kwanza kabisa ni kitu cha kukubali ya kwamba Apple ya chini ya uongozi huu imekuwa ya kitofauti na isiyotabirika kirahisi kama ya chini ya Steve Jobs. Na hivyo ni rahisi wao kuamua kuja na ata kitu kingine tofauti na kisichotegemewa kama gari, iCar.
Pesa wanazo ata za kununua kampuni kubwa ya magari ya umeme (electric cars) ya Tesla. Ila je ni kweli Apple wanaweza kuamua kuja na gari lao wenyewe kabisa ndani ya miaka hii michache kufikia 2020 kama watafiti wengi wanavyodai? Sidhani.
Je suala hili limeanzaje?
Madai ya kampuni hiyo kuwa inaweza ikawa mbioni kutengeneza magari yalianza kutolewa na mtandao wa 9to5Mac baada ya kufanikiwa kuorodhesha idadi kadhaa ya wafanyakazi walioajiriwa hivi karibuni ambao wanatokea katika ujuzi wa masuala ya utengenezaji magari na teknolojia ya magari yatumiayo umeme badala ya mafuta. Na siku chache zilizopita jarida maarufu sana duniani la Bloomberg nalo liliripoti kuwa kuna uwezekano kampuni ya Apple ikaleta gari, yaani iCar katika kipindi hiki cha hadi mwaka 2020.
Mpango wao huu wa teknolojia ya gari imepewa neno siri la ‘Project Titan’
Je litakuwa jambo la maana wao kujiingiza katika utengenezaji wa magari?
Ingawa hisa za kampuni hiyo zilipanda na kuweka rekodi ya juu kabisa baada ya taarifa hizi kuanza kusikika watu wengi ikiwa ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni kubwa ya utengenezaji wa magari ya GM Motors, Bwana Dan Akerson alisema kwa Apple hautakuwa uamuzi wa busara kujiingiza kwenye jambo ilo.
Bwana Akerson amedai biashara hiyo ni ngumu sana hasa kwa kuanzia, kwani kuna taratibu nyingi za kisheria na kiteknolojia zitakazopoteza muda mwingi na pesa nyingi, wakati huo huo biashara ya utengenezaji magari inatumia mtaji mkubwa wakati inatoa faida ndogo kwa wakati (low profit margin). Bwana Akerson anasema kwamba kwa faida ambayo kampuni ya Apple inapata kwa kila simu moja inayouzwa kujiingiza kwenye biashara ya utengenezaji magari hautakuwa uamuzi wenye faida.
Kampuni nyingine kubwa ambayo imekuwa imejikita kwa miaka kadhaa sasa katika teknolojia za magari janja ni Google. Hadi sasa gari lao linaloweza kujiendesha lenyewe limeshapitia hakiki mbalimbali na kupewa kibali cha kutumika kimajaribio zaidi. Google wametumia miaka mingi kufanikisha hili, je Apple wataleta teknolojia ya magari au watatengeneza magari? – Tutafahamu!
‘In-Car Technology’
Kama watu wengi wengine Bwana Akerson anaona sehemu muhimu zaidi kwa kampuni hiyo kujikita ni katika teknolojia nyongeza katika magari (in-car technology). Wengi pamoja na sisi TeknoKona tunaona uamuzi mzuri na wenye faida kwa kampuni ya Apple ni kujikita katika kubuni na kutengeneza teknolojia ya kutumika kwenye magari ambapo baadae wao waingie kwenye mkataba na makampuni mengine ambayo tayari yanatengeneza magari kama vile BMW, Toyota, GM Motors na wengine.
Bwana Akerson aliweka historia katika uongozi wake wa GM Motors kwa kampuni hiyo kuingiza gari lenye teknolojia ya intaneti ya 4G na hivyo kukuwezesha kupata huduma ya intaneti kwa mfumo wa WiFI kokote ukiwa na gari hilo. Ni teknolojia kama hizi ndizo zinazotegemewa kwenye magari ya miaka ya baadae. Uwezo wa kuweza kuwasaliana na simu janja yako n.k.
Hadi sasa mradi wa Titan unaendelea kuwa wa siri lakini mwisho wa siku tutakuja kujua kama wameamua kutengeneza gari kabisa, yaani iCar, au wameamua kutengeneza teknolojia nyongeza kwa ajili ya magari janja (smart cars).
Uwezo wanao!
Hadi kufikia Desemba mwaka jana kampuni ya Apple inazaidi ya Tsh trilioni 325 benki, (Dola bilioni 178 za Marekani), (bajeti ya serikali yetu kwa mwaka 2014/15 ni Tsh trilioni 19.6, unaweza pata picha ya utajiri wao hapo). Kwa utajiri huu wa fedha unawafanya kuwa na uwezo wa ata kununua kampuni kama ya Tesla Motors ambayo tayari imeanza kufanikiwa katika kutengeneza magari mazuri yatumiayo umeme. Kama kampuni ya Apple wakiamua kununua kampuni hii ya magari itawabidi kutumia Dola bilioni 78 tuu kutoka kwenye dola bilioni 178 walizokuwa nazo kufikia Desemba 2014.
Muda utatuambia ila kwa sasa fahamu ya kuwa Apple tayari wameshajiingiza kwenye masuala ya magari, lakini kama kawaida yao bado kuna usiri mwingi kuhusu ni hasa wanafanya.
No Comment! Be the first one.