Huawei wajikuta wakiomba radhi baada ya kuweka picha hii kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii. Je nini kilichokosewa katika picha hii?
Picha hii iliwekwa siku chache zilizopita katika kuitangaza na kuisifia simu yao mpya ya Huawei P9 yenye uwezo wa juu katika teknolojia ya upigaji picha.
Simu hii inakuja na kamera kutoka moja ya kampuni nguli katika masuala ya teknolojia ya kamera – kampuni inayofahamika kwa jina la Leica.

Picha hiyo inayoonesha ilipigwa kipindi jua likiwa linazama ni picha yenye ubora wa hali juu. Kama wewe ni mpenda kupiga picha basi picha hiyo na maneno yaliyowekwa katika post ya Huawei ikionesha ni picha iliyopigwa na Huawei P9 basi inaweza kukufanya kwenda dukani mara moja kununua simu hiyo.
Tatizo ni nini hasa?
Ni uongo!

Picha waliyoiweka haijapigwa na kamera ya simu ya Huawei P9, wajanja wa masuala ya mtandao waliweza kuichukua picha hiyo na kisha kuisoma data zake za kiundani na hapo ndipo walipokuta data zikionesha picha hiyo ilipigwa kutumia kamera ya hali ya juu tuu katika masuala ya upigaji picha ya Canon EOS 5D Mark III.
Kamera hiyo inauzwa kwa gharama ya zaidi ya dola 2500 ikiwa mpya (Zaidi ya milioni 5 za Kitanzania). Hichi ni kiwango cha juu sana ukilinganisha na bei ya Huawei P9 ambayo inacheza kwenye Tsh Milioni 1 na ushee…

Wajitetea
Huawei wameondoa post hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii na kisha kuomba radhi huku wakisema picha hiyo ilipigwa na kamera ya Canon kipindi wakipiga picha kwa ajili ya kuitangaza simu hiyo. Waomba radhi huku wakisema maneno yaliyowekwa kuambatana na picha hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii hayakuwa sahihi.
Soma kuhusu Huawei P9 -> HAPA
Upo hapo? Kuwa makini na picha za matangazo ya bidhaa, kumbuka mara nyingi unachoona si uhalisia..
Vyanzo: DailyStar UK na mitandao mbalimbali