Wakati Google wanajiandaa kutambulisha rasmi toleo jingine la Android wengi wanaona ni jambo lisilo na ulazima kwani bado toleo la sasa, Android Marshamallow ata halitumiwi na wengi.
Katika tukio linalotambulika kama Google I/O litakalofanyika baadae mwezi huu Google watatambulisha toleo la Android 7. Google I/O… I/O = input/output na Innovation in the Open
Suala la kushindwa kufikisha updates (masasisho) za kisasa zaidi kwa simu zilizo kwa watumiaji ni changamoto kubwa kwa Google ambayo inauzi watumiaji wengi na inaonekana kuwa moja ya changamoto muhimu kutatuliwa kuhakikisha ukuaji wa Android.
‘Fragmentation’ tatizo kubwa kwa watengenezaji apps (developers)
Fragmentation ni nini?
Fragmentation katika Android ni neno la kiingereza linalotumika kuelezea hali ya kuwa na aina mbalimbali tofauti ya simu zinazotumia programu endeshaji ya Android. Yaani kuna watengenezaji wengi sana wa simu za Android na simu hizo zinatofauti ya vitu mbalimbali kama vile ukubwa wa vioo, uwezo wa teknolojia mbalimbali na juu ya yote simu hizo zinatumia matoleo tofauti tofauti ya Android.
Katikati ya mwaka jana kulikuwa na aina tofauti za simu za Android zaidi ya 24,000 na huku zikiwa zimetengenezwa na makampuni tofauti zaidi ya 1,000…Simu za Samsung zilishikilia asilimia 37.8 ya simu zote za Android – OpenSignal
Hali hii inafanya watengenezaji apps kuwa na kazi ngumu kuhakikisha apps zao zinafanya kazi katika simu zote…na ubaya ni kwamba matoleo mapya kabisa ya Android yanayoleta teknolojia mpya na nzuri zaidi ndio yanakuwa yanapata ugumu zaidi kusambaa kwa haraka.
Hili linatokana na nini?
Mfumo wa simu za Android kupata updates (masasisho) ni tofauti kidogo na ule wa Apple na programu endeshaji yake ya iOS. Kwa mfano toleo jipya la sasa la iOS 9 lililotolewa mwezi wa tisa mwaka jana tayari linatumika katika asilimia 84 za iPhone na iPads….wakati toleo la Android Lollipop lilitolewa miezi kama hii mwaka jana linatumika katika asilimia 9 tuu ya simu na tableti za Android.
Tofauti kuu ni kwamba Apple wenyewe ndio wanatuma updates kwenda kwenye simu na tablet zao moja kwa moja wakati kwa Android, Google wanatengeneza updates na matoleo mapya ya Android na kisha wanawapatia watengenezaji simu kama vile Samsung, HTC na wengine na kisha ni jukumu la watengenezaji simu hao kufanya maboresho wanayoyataka na kisha kusukuma updates hizo kwenda kwenye simu zao.
Ubaya hapa ni kwamba watengenezaji simu hawa wanataka kuuza simu mpya na kutengeneza pesa zaidi na hivyo utoa updates hizi kwa simu chache sana na uleta sokoni simu mpya tena za bei ya juu zikiwa na matoleo ya kisasa ya Android. Hili linafanywa na Samsung, na ata wengine pia..
Google pia huwa wanatoa simu zao zinazofahamika kwa jina la Nexus, simu hizi ndio zinazokuwa na uhakika wa kupata matoleo mapya ya Android muda mchache baada ya matoleo hayo kutoka…hii ni kwa sababu Google wenyewe ndio wanaosimamia suala hilo.
Je suala hili litatatuliwa lini?
Wengi wanaona njia pekee ya kuondoa tatizo hili ni kwa Google kutafuta njia ya kuhakikisha suala zima la kuupdate simu linatoka mikononi mwa watengenezaji simu. Changamoto ni kwamba kila mtengenezaji simu huwa anafanya maboresho spesheli ya muonekano wa Android na hivyo kuitaji kufanyia maboresho hayo kwa kila toleo jipya la Android kabla ya kulituma kama update kwa simu husika.
Kama Google hawatakuja na njia ya kuonesha wanahakikisha matoleo haya mapya ya Android yanazifikia simu mbalimbali ambazo tayari zinatumika basi kutafanya uamuzi huu wa kuja na toleo jipya la Android kila mwaka kuwa hauna maana kabisa. Ni bora matoleo hayo yawe yanakuja kila baada ya miaka miwili au mitatu.
Je wewe unatumia simu ya Android? Unafahamu ata simu hiyo inatumia toleo gani? Tupe maoni yako juu ya hali hii ya ugumu wa kupata matoleo mapya ya Android kwa simu yenye sifa nzuri tuu.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa taarifa kutoka OpenGraph