Wakati bado tunasubiri huduma ya SMS katika Messenger (Huduma ambayo ilikuwa inafanyiwa majaribio kwa watumiaji wachache mwezi uliopita), Facebook wameleta toleo jipya la Messenger ambalo limekuja na muonekano tofauti naule tulio kuwa tunatumia awali.
Messenger ni app ya Facebook ambayo inatumika kutuma meseji za Facebook, huku ikiwa ni moja ya app ambazo zinawatumiaji hai wengi zaidi.
Muonekano huu mpya umefuata zaidi sheria na taratibu za ubunifu ulioletwa na Google ufahamikao kama ‘Material Design’
Toleo hili jipya la Messenger ni matokeo ya fununu na tetesi ambazo zilianza kusikika mitandaoni mwanzoni mwa mwaka huu juu ya mabadiliko makubwa katika muonekano.
Toleo hili jipya litakuwa na ufuto wa blue iliyokoza juu ambayo itakuwa na vitufe kwa ajili ya Chat, Groups, Mpangilio na mengineyo. Kwa upande wa chini sasa kutakuwa na kitufe kimoja (kama kinaelea) tu kwa ajili ya kuanzisha Chat ama kupiga simu na mengineyo.
Akijibu comments za watu katika posti yake ya Facebook kuyatangaza mabadiliko hayo mkuu wa kitengo cha app hiyo bwana David Marcus amethibitisha kwamba mabadiliko haya yatapatikana kwa watumiaji wote baadae leo. Mabadiliko haya hata hivyo hayajaleta kitu chochote kipya ila ni muonekano tuu ndio mpya.
Sasisha (Update) App yako na kisha utuambie maoni yako Je ni muonekano mzuri ama vipi? tungependa kusikia maoni kutoka kwako.