Baada ya wachambuzi kufungua Galaxy S8, simu mpya kutoka Samsung wamegundua kwamba kampuni hiyo imewaonya watumiaji wake juu ya madhara yatakayotokea iwapo betri ya simu itachezewa na Mbwa.
Jambo hili limeripotiwa sana na mitandao ya teknolojia kwa kuwa sio jambo la kawaida sana kuona alama hiyo inayowaonya mbwa.

Je kwanini betri hii ni hatari kwa mbwa?!
Duru za kichunguzi zimeenda mbali na kueleza kwamba iwapo betri hii itachezewa na mbwa sio tu itamsababishia matatizo ya kiafya bali kuing’ata kutasababisha mgandamizo katika betri ambao utapelekea betri hiyo kulipuka moto, mlipuko huu utakuwa kama milipuko ile iliyotokea katika toleo lililopita la Note 7.

Je kwanini Samsung watoe onyo kama hili ambalo hawajawahi kulitoa kipindi cha nyuma?
inawezekana kwamba ingawa betri ya S8 sio rahisi kutolewa lakini Samsung wanakwepa uwezekano wowote wa kuingia katika kashfa juu ya usalama wa vifaa vyao ni kama mtu aliyeng’atwa na nyoka hivyo hata akiguswa na jani anashtuka.
Pia inawezekana kwamba Samsung wameanza kuwaomba LG wawasaidie katika kitengo cha betri kufuatia mkasa uliowakumba mwaka jana, hii ni kutokana kwamba ni LG pekee pia ambayo inatumia kibandiko kama hicho ambacho kinawaonya watumiaji juu ya betri hizo kuwa hatari kwa mbwa.
Je ipo haja ya mtumiaji wa kawaida kuwa na wasiwasi juu ya tahadhari hii ?
Kimsingi hakuna haja ya mtumiaji wa kawaida kuwa na wasiwasi juu ya habari hii labda kama utaifungua simu yako kubadili betri kitu ambacho Teknokona inakusihi kutokifanya kama hauna ujuzi wa mambo ya simu.