Dar ni mji unaokuwa kwa kasi kubwa kuliko miji yote Afrika. Hii ni kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Miji huu unavutia mashirika, asasi za kiraia na makampuni kufanya majaribio ya kiteknolojia kujaribu kujenga ramani ya mji huu ili kukabiliana na changamoto zinazokuja na ongezeko la watu. What3words na Dar Ramani Huria ni kati ya jitihada zinazoweza kuiweka Dar kwenye ramani.
What3Words
What3words ni app inayolenga kutambua makazi yasiyo maalumu. Mtumiaji wa app hiyo atatumia maneno matatu kuweka kumbukumbu ya eneo fulani. What3words itatumia maneno hayo kurekodi ‘GPS cordinates’ – ambazo ni namba maalumu za kutambua eneo kwenye ramani, kwa usahihi wa mita 9 za mraba. Kama mtu huyo akitaka kurudi kwenye eneo hilo, anaweza kutumia tu maneno matatu kupata palepale anapotaka kufika. Kwa kugawanya dunia katika magridi ya mita 9 za mraba, What3words ina uwezo wa kutengeneza anuani trillioni 57 kwa kutumia maneno yote ya kamusi ya kiingereza. App hii imepata tuzo kubwa za ubunifu wa kiteknolojia za Tech Awards Silicon Valley – sehemu, ambayo ni kama makao makuu ya kampuni nyingi kubwa za teknoljia Marekani.
Anuani Zitasaidia
Serikali, mashirika na makampuni hutumia ramani katika kutambua makazi ya watu ili kutoa huduma. Kwa sasa suala la msingi linaloikabili nchi zinazoendelea ni kutambua makazi maalumu, au ya watu wasio na kazi maalumu, yani uswazi, ambao ni watu wengi zaidi. Kwa sasa, watu hawa wanakosa huduma muhimu za kijamii kwa sababu hawatambuliki wanapoishi. Kwa maneno ya Chris Shedrick, mmoja wa watengenezaji wa app hiyo, what3words ni suluhisho kwa tatizo kubwa la dunia.
Shedrick anaendelea kwa kusema, “Watu wataweza kufungua akaunti ya benki kirahisi zaidi kwa sababu wataweza kuelezea wanapoishi. Kama watahitaji msaada wa dharura, mamlaka zitajua wapi pa kufika. Wataweza pia kujisajili kwa daktari. Shule zitaweza kujua walipo wazazi. Watu wataweza kusambaziwa bidhaa majumbani kwao, kwani kutakuwa na njia rahisi kuwapata.”
Upo mfano uliopewa na BBC kwenye kipindi chao cha Click cha September 29, 2015 kinaelezea jinsi Chris alipoweza kufika kwenye mjengo wa BBC kwa kutumia app hiyo. Inaripotiwa pia, kwamba what3words itahitaji mtu, awe binafsi, kampuni au mamlaka awe na simu-janja na haitahitaji intaneti kufanya kazi.
Dar Ramani Huria
Programu nyingine inayotegemewa kuiweka Dar kwenye Ramani ni mradi unaoendelea hapa Dar es Salaam unaoitwa Dar Ramani Huria. Dar Ramani huria inatoa Ramani ya jiji Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuweka wazi maeneo yanayoweza kukumbwa na balaa la mafuriko. Kwa sasa, mradi huu unaofadhiliwa na benki ya dunia, unaendeshwa na jamii na kusaidiwa na wanafunzi wanaojitolea, ambao wanakusanya data muhimu na picha za maeneo ya jiji. Ndege ndogo isiyo na rubani (droni) inatumika kwenye mradi huu kuchukua picha za ramani kutoka mita 200 juu ya ardhi.
Ingawa Dar Ramani Huria ina malengo tofauti na kutengeneza mfumo wa anuani kwa mamilioni ya wana-Dar-es-Salaam wanao ishi kwenye makazi yasiyo maalumu, ramani hiyo na data zake inapatikana bure kwa mtu yeyote aanayetaka kuitumia kufanya hivyo.
Tukiangazia Mbele
What3Words wako kwenye mazungumzo na serikali 3 za Afrika kuona jinsi gani app yao itaweza kutumika rasmi kwa ajili ya anuani kwa Afrika. Halitakuwa jambo rahisi kupata mfumo wa anuani za watu wa makazi yasiyo maalumu lakini jitihada za dhati tayari zinafanyika kuelekea dira hiyo. Kwa mujibu wa Patricia Vivas, mtaalamu wa masuala ya anuani kwenye shirika la Posta katika Umoja wa Mataifa (UN Universal Postal Union), Tanzania ipo tayari kufanya hilo. Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, viongozi wamekuwa wakiwashirikisha wananchi na wadau muhimu kupata suluhisho la anuani kwa makazi yasiyo maalumu. Changamoto inayokuja ni kuona jinsi gani wananchi watakavyotumia nyenzo hizi kwa ajili ya maendeleo yao.
Chanzo: Mark Anderson in Dar es Salaam, theGuardian (UK), BBC Click (Sikiliza).
No Comment! Be the first one.