Kwa watu wengi sana simu janja zao ndio kila kitu (ukitaka kuamini angalia sura zao pindi wanapoibiwa) unaweza kutumia simu hizo kufanya karibia kila kitu
Kuanzia kwenye kufanya manunuzi ya vitu,kuelekezwa mitaa, kuangalia barua pepe na hata kuwasiliana na ndugu pamoja na jamaa. Mambo ya kufanya na simu janja ni mengi sana hata nikitaja sitayamaliza.
Ukiachana na kila kitu ambacho simu janja yako au tablet inachoweza kufanya inabidi uhakikishe kuna App za muhimu katika simu yako ambazo zitarahisisha ufanyikaji wa mambo hayo kwa namna ya kipekee.
KUTAFUTA SIMU ILIYO POTEA/IBWA
Hivi unajua hakuna mda mzuri wa kuibiwa? Chochote kama kweli ni chako kikiibiwa lazima uumie sana. Nshashuhudia dada kaibiwa simu akaanza kulia! (hizi smatifoni bwana, Hah!). hapo awali ilikua kama mtu ukiibiwa au ukipoteza simu yako matumaini ya kuipata tena hakuna kabisa
Lakini asante kwa Find My iPhone (ya iOS) na Android Device Manager (ya android) sasa tuna matumaini ya kupata vitu vifaa vyetu. Kwa kutumia App hizi kuna hati hati kuwa tunaweza kupata vifaa vyetu kwakufatilia nyendo za simu zetu zilizopotea/ibwa
Kama App hizo mbili hazitoshi kuna App nyingine inaitwa Prey, ambayo ni moja kati ya App nzuri za ulinzi na usalama. Prey inatuma eneo (location) ambalo simu yako iliyoibiwa ipo. Inaweza pia hata ikapiga picha kwa baadhi ya vifaa kwa kutumia kamera ya mbele lengo likiwa ni kukutumia picha ya mwizi wako. Pia utaweza kujua kama mwizi wako anajaribu kubadilisha laini katika simu. Lakini kama unaona kama haitoshi unaweza ukafuta kila kitu ukiwa mbali na simu hiyo.
PANGILIA PICHA ZAKO
Kama una simu janja hiyo haina ubishi kuwa kuna picha nyingi sana katika simu hiyo. Kutokana na kuwa na picha nyingi kiasi hicho kuzipata zile ambazo unataka kutuma kwa familia na marafiki ni kazi kidogo na hauwezi kufanya jambo hili kwa haraka. Pia ukiweka picha nyingi sana katika simu yako unaweza ukapata kale kaujumbe ka “Not Enough Storage Space” kakiwa kanamaanisha kuwa uhifadhi hautoshi.
Chukua ukurugenzi katika picha zako kwa kutumia App kama Tidy au Sortpad. App hizi zinakuwezesha kupangilia picha zako katika ma’Folder’ tofauti au hata kwa makundi vile wewe utakavyo amua. Vile vile unaweza amua kufuta baadhi ya picha kirahisi
Kinachofuata kama kuna picha ambazo usingependa kuzipoteza milele unaweza ukazihifadhi katika huduma ya hifadhi ya mtandaoni (cloud service). Google Photos na Room For More yanaweza yakawa machaguo sahahi kwako.
TAFUTA WiFi
Mara nyingi tuu inatokea , kipindi ambacho unataka WiFi kwa hali na mali lakini huweza kupata huduma hiyo kwa sababu tuu umelipita eneo lake linalotakiwa. Hii inaweza ikakutokea wakati unafanya mambo yako kwa mfao ukiwa unatumia kivinjari kuperuzi katika mtandao, mara kitu kinakata!. Najua kila mda mtandao unapokata kisa tuu umepita wigo wa kutumia WiFi unakua unaudhika kwa kiasi chake.
Kwa kutumia WiFiMapper utakuwa na mkombozi linapokuja swala zima la kutumia WiFi. Kwa kutumia App hii unaweza kutafuta na kubaini WiFi ambayo inafaa kutumiwa kati ya zote zilizopo katika eneo hilo.Unaweza ukagundua WiFi zilizo wazi lakini zenye usalama mzuri tuu. Ukiwa na App hii utapata huduma ya kimtandao na hautacheza mbali na App zako muhimu kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp.
Pia usipate hofu kwamba huenda unaweza ukajiunga na WiFi ambayo ina madhara. Kwani WiFiMapper itakuambia kabisa kwamba mtandao ni wa aina gani.
Pakua WiFiMapper hapa kwa iOS na Android na baada ya hapo hautakua na haja ya kukosa mtandao wa intaneti katika simu yako.
LINDA MB/GB ZAKO ZA INTANETI
Mpaka ikaitwa simu janja ina maana inaweza fanya kazi nyingi sana. Lakini lazima tujue kwamba kazi nyingi katika simu janja zinahitaji uwepo wa mtandao wa intaneti. Fikiria App zako kama vile WhatsApp, Facebook na App zingine nyingi bila intaneti sio kitu tena.
Fikiria kutazama video katika Youtube, kwa kifupi yote haya yanahitaji utumie inteneti yako. Kama una MB/GB za mawazo inaweza ikawa ni shida kwako kwani utapata tabu katika kupangilia kipi utumie na kipi usitumie. Mda mwingine MB/GB zako zitaisha kabla ya muda ambao uliutegemea.
Kuna namna nyingi tuu na tofauti tofauti ambazo unaweza ukaishiwa MB/GZ zako lakini kwa kutumia App ya Onavo Extend inaweza ikakusaidia katika hili. App hii kazi yake ni kufinya ‘Data’ ambapo itakuwezesha kupata hadi mara tano ya utumiaji wa MB/GB zako (haimaanishi kama ukitumia App hii kama ulikua na GB 1 utapata GB 5). Kama simu yako ina uweza wa WiFi basi app hii itakuunganisha automatiki ili kuhakikisha una sevu MB/GB zako.
Pia App hii inaonyesha picha ambazo unataka kuziona tuu, kwa mfano ukiwa mtandaoni haitafungua picha za chini kabisa ambazo hujazifikia. Unaweza ukashangazwa vitu vidogo kama hivi vinasevu ‘Data’ zetu kwa kiasi gani. Pia app hii itakupa ripoti ya mwezi ili kujua ni App gani zinatafuna MB/GB zako kwa sana.
LINDA BETRI LAKO (UWEZO WA KUKAA NA CHAJI)
Simu janja zetu zinafanya vitu vingi sana na vitu vingi vinachukua sehemu kubwa ya chaji.Hebu fikiria ni App ngapi katika simu yako zinafanya kazi hata kama hujazifungua na kuzitumia (background refresh) zenyewe.Kuna App ambazo pia mara kwa mara zinaangalia eneo gani ulilopo, hata mwangaza katika simu yako ni baadhi ya vitu tuu ambavyo vitaweza kumaliza chaji ya kifaa chako.
Ndio maana hata katika simu za iPhone ambazo zina matoleo ya program endashaji za sasa zaidi zina kitu kinaitwa “Low Power Mode” kwa lengo la kuongeza uhai wa betri.
Kama unahitaji msaada mzuri tuu katika uhai wa betri lako kwa simu za iOS na Android basi App ya Battery Doctor ndio jibu.
Battery Doctor kazi yake ni kusimamia Betri la simu janja yako. Hii inamaanisha kuwa betri lako halitakufa(isha chaji) kirahisi pale unapolihitaji kwa hali na mali (labda chini ya 10%). Kwa kifupi App hii itaweza kuendesha mfumo mzima wa betri katika simu janja yako.