Muda unakimbia kweli kweli… Twitter yafikisha miaka 10 tokea mtandao huo wa kijamii kuanza kupatikana – ulianza rasmi Machi 2006. Je utaendelea kuwepo miaka 10 ijayo?
Hili ni swali gumu kulijibu, miaka 10 ya Twitter imekuwa yenye mafanikio na changamoto mbalimbali. Ili kuweza kujua kama utaendelea kuwepo ni vizuri kuangalia historia ya mitandao mingine ya kijamii maarufu.
Angalia hali ilivyokuwa kwa mitandao mingine 2 ya kijamii pale ipofikisha miaka kumi.
Myspace – Kuazishwa mwezi wa nane, 2003
Kama kuna mtandao uliobomba kwa sana katika miaka ya mwanzo ya ukuaji wa mitandao ya kijamii basi ni mtandao wa mySpace.
Mtandao wa MySpace ulianza rasmi mwaka 2003 mwezi wa nane. Na ndio ulikuwa mtandao mkubwa wa kijamii kabla ya ujio wa Facebook, na inasemekana kuna kipindi – mwezi wa 6, 2006, mtandao huo ulitembelewa mara nyingi kuzidi ata mtandao wa Google kwa wakati huo.
Baada ya miaka mitano ya uwepo wake tayari ukaanza kupoteza umaarufu, hasa hasa kwenye ukuaji wa watumiaji…mwaka 2008 ukapitwa kwa mara ya kwanza na Facebook. Kufikia miaka yake 10, hii ikiwa ni 2013 mtandao huo wa kijamii tayari ulikuwa mahututi kiasi cha kuuzwa kwa Justin Timberlake ambaye naye alijaribu kuufufua upya lakini ikashindikana.
Mwezi wa pili mwaka huu mtandao huo uliuzwa tena kwa kampuni ya Time lengo likiwa si kuufufua bali ni kutumia data mbalimbali za watumiaji wake wa kuanzishwa kwake kwa ajili ya maboresho ya kimatangazo… Kuna utani mtandao huo umeuzika kama ‘skrepa’ 🙂
Facebook – Kuanzishwa mwezi wa pili, mwaka 2004
Mtandao wa kijamii wa Facebook ndio mtandao mkubwa zaidi wa kijamii kwa sasa – na hakuna ambao uliokwishawahi fikia idadi ya watumiaji kama Facebook.
Data zinaonesha mtandao huwa unawatumiaji zaidi ya bilioni moja. Mtandao wa Facebook ulifikisha umri wa miaka 10 mwaka 2014 na katika kipindi chote cha mwaka huo kulikuwa na wastani wa watumiaji bilioni 1 kila mwezi kwenye mtandao huo.
Mtandao huu unakua ingawa kuna wasiwasi juu ya vijana wapya kama wataendelea kuupendelea mtandao huo – kuepuka wazazi wao..ambao wengi wao washakuwa watumiaji wa muda mrefu wa mtandao huo.
Kuna tafiti mbalimbali ambazo tayari zinaonesha vijana wadogo siku hizi wanatumia muda mwingi zaidi katika huduma zingine kama vile Snapchat, Instagram n.k, ila kwa kiasi kikubwa Facebook wataendelea kuwa salama kwani tayari wanamiliki huduma zingine kubwa kama vile Instagram, na WhatsApp.
Bado ni mapema sana kuona ushukaji wa utumiaji kwa mtandao wa Facebook…
Twitter – Muhimu kujifunza ni kipi kinawapendeza watumiaji wake
Wengi wanaona kitu muhimu kikubwa katika kujihakikishia ya kwamba mtandao wa Twitter kutokuwa historia kama ilivyo kwa MySpace, Hi5, tagged na mingineyo ni kwa mtandao huo kuhakikisha haufanyi mabadiliko yasiyokubalika na watumiaji wake.
Tayari mara kadhaa fununu za mabadiliko kama vile uondoaji wa kikwazo cha herufi 140 n.k zimekuwa zikileta mazungumzo makali ya upingwaji huku hashtag ya #RIPTwitter ikitumika.
Tayari mitandao ya Facebook na Twitter inaonekana imekuwa mikubwa na yenye nguvu kiasi cha kufanya mitandao mingine ya kijamii yenye sifa sawa kuwa vigumu kuanzishwa. Unaikumbuka Google Plus?
Kwa sasa uhakika wa kudumu kwa mitandao hii ni kuhakikisha ukuaji katika upatikanaji wa watumiaji wapya pamoja na kufanya wenye akaunti kuendelea kuitumia…hayo mawili pamoja na kuwa na mabadiliko yanayowafurahisha watumiaji ndio vitu muhimu katika kujihakikishia ya kwamba wataendelea kuwepo.
Miaka 10 ni mingi sana na Twitter wanastahili pongezi….wajifunze na kuendelea kupiga kazi kujihakikishia kuwepo tena miaka 10 ijayo.
Vyanzo: Twitter, Newstatesman.com, Google Trends