Shirika lisilokuwa lakiserikali la internet.org duniani limeungana na Airtel ya Zambia kuwapa watu wa Zambia internet ya bure kabisa kwa huduma chache za msingi na zile zinazotumika na watu wengi duniani kama facebook.
Shirika hili linapewa msaada na kampuni ya Facebook na lina ndoto ya kuunganisha dunia nzima kwa intaneti. Watu nchini Zambia hivi sasa wanapata huduma za bure za intaneti kupitia app mpya inayobeba jina la ya shirika la internet.org. App hiyo inapatikana kama app ya kawaida, kama app ndani ya facebook na pia bure kabisa kwenye mtandao kwenye kisakuzi (browser) cha simu za zamani, zenye uwezo mdogo wa intaneti.
Imetambulika kuwa asilimia 85 ya billioni 5 ya watu duniani hawawezi kununua mpango wa intaneti (bando) na hivyo kukosa kutumia huduma hiyo. Kwa kuzingatia hiyo, harakati hizi za intaneti ya bure zinatazamiwa kusaidia kuwafikishia watu huduma hii na hasa huduma za msingi kama wikipedia, google ya kutafuta, messenger na huduma za ya afya, elimu, kazi, hali ya hewa, serikali na msaada wa kisheria kwa wakinamama.
Baada ya kuanza kutoa huduma hiyo kwa Zambia, shirika linategemea kupeleka huduma hiyo katika nchi nyingi zaidi barani Afrika, Asia na Marekani ya kusini. Cha kushangaza ni kwamba katika kufanikisha intaneti ya bure, gharama hazitabebwa na internet.org wala Facebook – zitabebwa na makampuni ya mawasiliano. Usishangae. Ujanja ni kwamba, inatazamiwa kuwa kwa kupitia huduma hizi za bure, watu watapata hamasa ya kulipia zaidi kutumia huduma zingine za intaneti. Hapo makampuni hayo yataweza kupata wateja wapya na kuingiza faida zaidi.
Wachambuzi kadhaa wanaishutumu Facebook kwa kujipanua kiujanja. Hii siyo mara ya kwanza kwa kampuni ya Facebook kushinikiza intaneti ya bure na kwamba siyo kampuni pekee yenye mtazamo huo. Kampuni ya Google pamoja na hata watu binafsi nao wako kwenye harakati tofauti kuwezesha dunia kupata intaneti ya bure lakini tayari Facebook imefanikiwa na ‘Project Facebook Zero,’ mradi ambao unaoendeshwa pamoja na makampuni ya simu za mkononi za hapa Tanzania, huko Ufilipino na Paraguay tangu mwaka 2010. Mwanzilishi na mtendaji mkuu wa Facebook, Mark Zuckerberg amekaririwa na mtandao wa TechCrunch akisema, “Mafanikio ya mradi huu yamezaa watumiaji millioni 3 wapya wa intaneti ” na kusema, “Tunaamini kuwa kila binadamu anapaswa kupata huduma za msingi za intaneti ikiwemo afya, elimu, kazi na mwasiliano.
Katika harakati nyingine, shirika la Internet.org kwa kushirikiana na Facebook na washirika wake wa mitandao ya mawasiliano, liko kwenye mchakato wa kuwapa intaneti kwa kutumia droni (ndege ndogo zisizoongozwa na rubani) na setelaiti asilimia 15 ya watu wasio na huduma hiyo kwa sababu ya umbali wa minara ya mawasiliano.
No Comment! Be the first one.