Windows Defender ni programu spesheli katika matoleo ya programu endeshaji ya Windows kuanzia toleo la Windows 8 – programu hii inalinda data na programu nzima ya Windows dhidi ya programu chafu maarufu kwa majina ya ‘malware’ na ‘virus’.
Na sasa Microsoft wametangaza kuipa uwezo mwingine mkubwa katika kuzuia na ata kufuta kabisa programu zinazojidai zinafanya kazi ya kukusaidia kusafisha mafaili ili kukuongezea ujazo wa diski (space) wakati ndio kwanza zinafanya kompyuta kuwa nzito.
Microsoft wamesema ingawa kuna programu chache zinazotoa ahadi ya uwezo wa kufanya kompyuta yako iwe bora zaidi kiutendaji zinafanya hivyo kweli ila nyingi sana hazifanyi hivyo kama zinavyoahidi. Matokeo zinaingiliana na utendaji kazi wa programu endeshaji ya Windows na hivyo kuifanya kompyuta yako kuwa nzito zaidi.
Na sasa wanachukua hatua kupitia kuipa uwezo programu endeshaji ya Windows Defender. Uwezo wa kuzigundua na kuziondoa. Na programu hiyo itakusaidia kuondoa ata zile programu zinazojidai kugoma kutoka hata baada ya wewe mwenyewe kuzi-uninstall kupitia eneo la Programs.
Historia ya Windows Defender
- Windows Defender ilianza kutolewa na Microsoft bure – Free Download, enzi za Windows XP ikiwa ni programu spesheli dhidi ya udukuzi wa kufuatiliwa tuu (spyware). Ila na muda Microsoft wameibadilisha na kuipa uwezo mkubwa zaidi.
- Kuanzia toleo la Windows 8 Microsoft walifanya uamuzi wa kuipa programu ya Windows Defender uwezo mkubwa dhidi ya virus, kazi iliyokuwa inafanywa na programu mbalimbali za kununua (anti-virus) hii ikiwa ni pamoja na ya kwao ya bure iliyojizoelea umaarufu walipoitoa kwa ajili ya kompyuta zinazotumia Windows 7 – Microsoft Security Essential (ilikuwa bure).
- Kuanzia Windows 8 Microsoft waliachana na programu ya Microsoft Security Essential, na kutumia mafanikio yao katika programu hiyo ya Anti-Virus kuboresha na kuja na Microsoft Defender ambayo inakuja moja kwa moja na programu endeshaji kuanzia Windows 8 bila uhitaji wa mtumiaji kuishusha (download).
Windows Defender huwa inafanya kazi nyuma ya pazia kuhakikisha hakuna programu chafu (malware/virus) anayetaka kuathiri kompyuta yako. Na kupitia watafiti mbalimbali imekwisha onekana ya kwamba programu hiyo inafanya kazi kwa ubora mkubwa tuu na ata kuzipita baadhi ya programu nyingi za AntiVirus zinazouzwa kwa gharama kubwa.
Kumbuka: Ukiwa unatumia programu ya Windows Defender hutakiwi kuweka programu nyingine ya AntiVirus. Mara zote ni programu moja tu ya Antivirus inatakiwa kutumika katika kompyuta yako. Zaidi ya hapo zitakuwa zinaingiliana na kuzidi kuathiri kompyuta.
Chanzo: MarketExclusive.com na Microsoft