Toleo jipya la programu endeshaji ya bure ya Ubuntu laanza kupatikana kupitia mtandao wao na TeknoKona tutakuelezea machache muhimu ya kujua kuhusu toleo hili jipya la Ubuntu 16.04 LTS
Majina ya matoleo ya Ubuntu
- Matoleo ya programu endeshaji ya Ubuntu yanatoka kila mwezi wa nne na kumi wa kila mwaka. Na majina yake ya mwisho yanabeba mwaka na mwezi wa toleo, yaani 16.04 ni mwaka 2016, mwezi wa nne.
- Na LTS inasimama kwa matoleo makuu ambayo mtumiaji ataweza kuyatumia kwa hadi miaka minne bila shida yeyote, utatakiwa tuu kupakua masasisho (install updates) za ulinzi na usalama.
- Ubuntu ni programu endeshaji inayopatikana bure kabisa kwa watumiaji wote na ni mbadala wa programu endeshaji ya Windows.
Nini kipya katika Ubuntu 16.04 LTS
Hakuna tofauti sana kubwa na toleo la Ubuntu 15.10 lilotolewa mwishoni wa mwaka jana. Kikubwa katika Ubuntu 16.04 LTS ni maboresho makubwa ya kimuonekano (kimombo – polish), maboresho haya yanafanya programu endeshaji hiyo kuwa ni ya kimvuto zaidi ukilinganisha na matoleo ya zamani.
Kwa miaka mingi wengi wamekuwa wakiona programu endeshaji za Linux kama vile Ubuntu zinakosa mvuto wa kimuonekano na ilo ndilo linalofanyiwa kazi sana na timu ya Ubuntu kwa sasa.
Launcher sasa itaweza kuhamishwa!
Katika mabadiliko yaliyowauzi wengi wa watumiaji wa Ubuntu miaka ya nyuma ni pale ambapo muonekano wa desktop wa Unity ulipoletwa na kulazimisha launcher (sehemu ya kubofya kuona apps n.k – kama ‘Start’ kwenye Windows) kuwa upande wa kushoto tuu. Kwa sasa watumiaji wa Ubuntu wataweza hamisha launcher na kuweka upande wa chini badala ya kushoto tuu kama ilivyokuwa zamani.
Ubuntu Software Center imeagwa rasmi – Karibu GNOME Software Application
Soko la kutafuta na kupakua apps za kutumika katika programu endeshaji hilo la Ubuntu Software Center limeacha kutumika na kuanzia sasa Ubuntu nao watakuwa wanatumia Gnome Software Application – soko hili la apps la Gnome ni maarufu kwa ata familia zingine za programu endeshaji za Linux kama vile Fedora.
DEB packages? — kwa miaka mingi watu wamekuwa wakiweza kupakua apps/programu kwenye Ubuntu kwa kutumia mafaili spesheli ya DEB (Haya unaweza linganisha na mafaili ya .exe kwa programu endeshaji ya Windows na apk kwa Android). Kuanzia toleo hili Ubuntu ina’support’ pia mfumo mpya wa mafaili yajulikanayo kama Snaps. Mfumo huu ni bora zaidi ukilinganisha na wa DEB.
Watumiaji wa kadi za AMD – habari njema!
Watumiaji wa kompyuta zinazotumia kadi za AMD na wao kwa sasa watapata haueni kwani Ubuntu 16.04 LTS inatambua kadi nyingi zaidi za AMD na hivyo shida ya upatikanaji wa ‘drivers’ si mkubwa kama zamani. Ila bado maendeleo zaidi yanaitajika ukilinganisha na wale wanaotumia NVIDIA – za Nvidia nyingi zinapata support kwa muda mrefu kwenye Ubuntu.
Unaweza download toleo la Ubuntu bure – www.ubuntu.com