Mamilioni ya simu za Android hatarini dhidi ya udukuzi kutokana na matatizo kwenye teknolojia ya chip.
Shirika linalojihusisha na masuala ya tafiti za kiusalama za mifumo ya kimtandao, Check Point iliweza kuona tatizo hilo na kutoa taarifa ambazo zilifanyiwa kazi na shirika la Qualcomm Disemba mwaka jana.
Check Point wameiweka taarifa hiyo wazi kwa mara ya kwanza, wakiamini tatizo lililokuwa linafanya usalama wa simu hizo kuwa chini litakuwa lishafanyiwa kazi kupitia masasisho ya programu endeshai ya Android ambayo yameshatoka kuanzia mwezi Disemba.
Fahamu zaidi kuhusu Chip – Chip ni nini?
Qualcomm ni moja ya makampuni makubwa duniani yaliyojikita katika utengenezaji wa chip zinazotumiwa na mamilioni ya simu. Chip hizi ndizo zinazosimamia teknolojia mbalimbali kama vile za mitandao ya simu – mawasiliano, kamera na mengine mengi.
Tatizo lilikuwaje?
Check Point walitambua kuna tatizo kwenye eneo la chip linalosimamia mawasiliano ya simu ‘mobile station modem’. Kupitia eneo hilo mdukuzi angeweza kupata uwezo wa kudukua simu ya mtumiaji yeyote duniani. Hii ni pamoja na uwezo wa kuweza kufungua PUK ya laini, kuweza kuona taarifa za simu na ujumbe mfupi unaoingia na pamoja na kuweza kudukua mazungumzo yanayofanywa kupitia simu husika. Robo ya simu zote za Android zinazotumika hadi sasa zinatumia aina hiyo ya modem katika Chip za Qualcomm.
Baada ya Check Point kufahamu hili kupitia tafiti zao, walipeleka taarifa zao kwa kampuni ya Qualcomm ambao waliifanyia kazi mara moja. Hii ilihusisha wao kutengeneza masasisho spesheli ambayo yalitumwa kwenda kwa makampuni yanayotengeneza simu yanayotumia chip hizo; makampuni hayo ni pamoja na Google kupitia simu za Pixels, pia wapo Samsung, LG na wengine wengi.
Fahamu ni muhimu sana kuendelea kusasisha apps na programu endeshaji yako ya simu kila unapopata taarifa ya kufanya hivyo. Mara nyingi kunakuwa na masasisho yanayoboresha usalama wa vifaa vyako vya elektroniki na data zako kwa ujumla.
Chanzo: CheckPoint
No Comment! Be the first one.