Mwezi wa nne niliandika kuhusu hali ngumu kimauzo iliyokuwa inaikabili kampuni ya RIM (Research In Motion) watengenezaji wa simu maarufu za Blackberry, niliandika ‘RIM; Je Kifo Cha Kampuni ya BlackBerry Kinakaribia’.
Hali mbaya bado inaendelea na sasa imefikia hatua wamesukuma mbele muda wa kuziingiza sokoni simu za kisasa zaidi za Blackberry 10
ambazo wengi wamekuwa wakiziona kama ndo zitakazoweza kuleta ushindani kidogo katika soko linaloshikiliwa na simu za IPhone na zile zinazotumia Android kama Samsung, Motorola na wengine.
Lakini baada ya kupata hasara ya zaidi ya bilioni 500 katika kipindi cha miezi ya Aprili, Mei na Juni kampuni ya RIM imetangaza kupunguza wafanyakazi takribani 5000 na zaidi ya yote kutoziingiza sokoni simu za Blackberry 10 mwaka huu.
Hivyo kwa wale walioanza kuzitamani ni kwamba itabidi mvumilie hadi mwakani hapo kampuni hii itakapoweza kuwa katika hali nzuri ya kuweza hadi kupiga promo la nguvu ili muweze kuzipata simu hizi zinazosemekana kuwa ndo nguvu za mwisho za kampuni hii kubakia katika ‘game’. Kwani hadi sasa kuna uvumi wamiliki wanafikiria ata kuuza kampuni hii mapema zaidi kabla mambo hayajakuwa mabaya. Wakati huo huo watafiti wengine wanashauri ni bora kampuni hii ijikite katika soko la maofisi zaidi wakati wengine wanaona njia pekee ni nao kutumia ‘operating system’ ya Android kutoka Google.
Simu Ya Blackberry 10 |
Mengi yataongewa, ila tutaona mambo yatakuwa vipi ndani ya kipindi hichi chote kabla ya simu za Blackberry 10 kutoka hapo mwakani, kwani mambo yanazidi kuwa mabaya sana kwa RIM. Hii ni pamoja na bei za hisa zake kuporomoka sana.
Muda ndo utakaotuambia, najua kwa Bongo sasa kama nchi nyingi nyingine zinazoendelea utumiaji wa Blackberry unakuja juu sana, na zaidi ya yote umekuwa kama fasheni; Je unatumia? Au unampango? Kwa sasa kampuni hii inaweka nguvu zaidi katika masoko ya nchi zinazoendelea baada ya masoko ya nchi zilizoendelea na hasa marekani na canada kutawaliwa na simu za Android na IPhones.
No Comment! Be the first one.