Droni, au ndege ndogo zisizokuwa na rubani zimekuwapo kwa muda mrefu sasa na pengine wengi wameziona zikifanya kazi hasa katika masuala ya vita – kwa mfano vita dhidi ya majangili hapa Tanzania.
Ukweli ni kwamba ni watu wachache tu wa kawaida wanaweza kuwa na taswira ya jinsi gani hivi vifaa vinaweza kuingia katika maisha yao. Hapa tunakuletea njia nne zinazoonekana kuwa na uhalisia siku za karibuni.
1. Droni zinazokuletea mzigo kutoka sokoni hadi Mlangoni kwako
Kama bado huna ufahamu, Amazon tayari wamekuwa wakifanya majaribio mengi tu ya kutumia droni za kutoa mzigo kwa wauzaji kupeleka kwa mnunuaji. Mfumo huo wanaoujaribu unaitwa Amazon Prime Air na ni wa kusafirisha mizigo kwa watu ndani ya dakika 30 za kununua.
Huduma hii inaonesha matumani ya kuwa kweli, kwani Amazon wameweza kupiga hatua kubwa ndani ya muda mfupi, ingawa changamoto lukuki bado zipo. Huduma hii na kama hizi zikifanikiwa, kuna matumizi mengi tu ikiwemo ya muhimu zaidi ya huduma za msaada wa kwanza.
2. Droni za Kusaidia Usalama
Katika kutumia kamera na droni, mambo mengi mema na ya kustaajabisha yanaweza kutokea ila suala la usalama ni linalotazamiwa zaidi. Fikiria kama utaweza kupata ushahidi wa picha kutoka popote bila ya kuwa mahala hapo. Wapo wanafikiria kwamba droni zinaweza kutumika katika maeneo ambayo yana historia mbaya ya usalama wa wananchi. Fikiria pia kama una sehemu yako kubwa kiasi, kama shamba ambalo ungependa ilindwe kwa gharama ndogo na uhakika, droni inaweza kuwa suluhisho zuri.
3. Droni za Kusaidia Kutafuta Mahali pa Kuishi
Yapo pia mashirika mengi yanayotamaani kutumia droni kuchunguza maeneo mazuri ya kuishi bila kutumia gharama na watu wengi. Kwa mfano, Uchina walitoa tamko wakiamua kutumia droni kutafuta suluhu ya tatizo lao la moshi wa mjini.
Matumizi ya droni ya namna hii yanaweza kuwa na manufaa binafsi kama kuamua kama unataka kuhamia nyumba husika au la kwa kuangalia picha kwa kutumia droni ya kampuni inayokuuzia nyumba.
4. Droni za Kutoa Huduma za Intaneti kama Minara
Mwaka 2015, facebook walitangaza kutumia droni za umeme-jua kusaidia kupeleka intaneti ya bei nafuu kwa nchi zinazoendelea. Droni hizo zenye uwezo wa kukaa futi 60, 000 – 90, 000 angani kwa miezi mitatu, zinauwezo wa kutoa intaneti ndani ya radius ya maili 50.
Mpaka sasa, droni ni kitu kinachoonekana kama kitu cha anasa ama pengine kitu cha mchezo na kujifurahisha ila kampuni nyingi zinaona kwamba matumizi ya droni yanaweza kumfikia mtu wa kawaida na kwa bei nafuu iku za mbeleni. Kwa mtazamo huo, usishangae kuona droni zikipata matumizi ya kila siku muda si mrefu.
Je, umewahi kuona droni? Umewahi kutumia? Tupe maoni yako.