Kampuni ya Microsoft imetangaza kuwa, kuanzia wiki lijalo itaacha kutoa masasisho (updates) kwa kivinjari chake cha Internet Explorer kwa matoleo ya zamani ya 8, 9 na 10.
Japo watumiaji wengi wa mtandao duniani wamekua wakishutumu matoleo hayo kuwa dhaifu katika kuperuzi mtandaoni, lakini kivinjari cha IE kimekuwa muhimili mkubwa kwa mamilioni ya watumiaji wa mwanzo wa huduma za mtandao.
Microsoft wameamua kuacha kutoa huduma kwa wateja pamoja na ulinzi kutoka katika kivinjari hiki, lakini si kwa kushitukiza. Tayari wameanza kutuma ‘notification’ tangu tarehe 12, January hii kwa watumiaji wa IE 8,9 na 10 kuweza kupakua kivinjari kipya cha IE 11. Ujumbe huo unawaelekeza watumiaji namna ya ku shusha IE11 pamoja na jinsi ya kuhifadhi mipangilio yake katika kompyuta.
Microsoft wamesema kuwa, IE 11 itamwezesha mtumiaji wa mtandao kuwa na uhakika wa Usalama wa data zake, uhakika wa kasi na uthabiti wa kazi, pamoja na kufanya kazi sambamba na mitandao mipya ya kisasa.
Zaidi ya asilimia 54 ya komputa bado zilikuwa zinatumia IE za zamani mpaka kufikia mwaka 2014. Hii haimaanishi kuwa, watumiaji watakapokiuka kushusha kisakuzi kipya watashindwa kutumia vya zamani, La Hasha! Wataweza kuvitumia, lakini kwa hatari ya kukosa usimamizi wa usalama wa data na marekebisho ya visakuzi hivyo.
Microsoft wanaeleza kuwa, watumiaji wa IE 11 watapata uzoefu unaokaribina kabisa na ubora wa kivinjari kipya cha Microsoft Edge kinachopatikana kwa watumiaji wa Windows 10.
Wengi wanaona uamuzi huu unaweza wapeleka watumiaji wa matoleo hayo ya Internet Explorer kujaribu vivinjari vya Firefox na Google Chrome. Ila haijalishi sana watatumia kipi ukweli ni kwamba ni muhimu sana kutumia matoleo ya vivinjari ya kisasa zaidi ili kuhakikisha data zako zinakuwa salama wakati wote ukiwa unatumia mitandao.
Chanzo cha habari hii ni Sci-Tech na Engadget.
No Comment! Be the first one.