Kampuni inayomiliki viwanda vinavyotengeneza simu za iPhone kwa ajili ya Apple, Foxconn, inasemekana ipo katika hatua za mwisho kuingia mkataba na serikali ya India kuweza kufungua kiwanda kikubwa cha utengenezaji wa simu za iPhone nchini India.
Katika ripoti iliyotolewa na ‘The Economic Times of India’, kampuni ya Foxconn imefanikiwa kupata eneo la eka 1,200 la ardhi katika jimbo la Maharashtra., magharibi mwa India.
Kampuni ya Foxconn ni ya nchini Taiwan na inamiliki viwanda vingi nchini China huku mteja wao mkubwa akiwa Apple
Inategemewa mara moja baada ya makubaliano kusainiwa utengenezaji wa kiwanda hicho utaanza mara moja, inategemewa hadi kukamilika kwa kiwanda hicho itachukua miezi 18, na kitagharimu takribani dola bilioni 10 za Marekani.
Kampuni hiyo inalenga kufungua viwanda 10 hadi 12 kufikia mwaka 2020, tayari mauzo ya iPhone mpya duniani yanashuka na inategemewa soko la India (nchi ya pili kwa idadi ya watu baada ya China) ni soko muhimu sana kwa Apple kama wanataka kuona mabadiliko katika mauzo yao.
Foxconn walikuwa na kiwanda nchini India kwa miaka mingi huku wakiwa wanatengeneza simu kwa ajili ya kampuni ya Nokia, ila kiwanda kilifungwa mwaka 2014 baada ya mkataba wao kukwama.
Kampuni ya Apple pia inajenga ofisi kubwa nchini humo katika jiji la Hyderabad, ofisi hiyo inayotegemewa kuwa na zaidi ya wafanyakazi 150 itajikita katika masuala ya mauzo na utengenezaji wa simu zake (kwa kiasi kikubwa inaonekana itakuwa kwa ajili ya kushirikiana na Foxconn pia).
Chanzo: IndiaTimes