Sio muda mrefu umepita tangu mwenzangu Hash aitambulishe Android 5.0 ‘Lollipop hapa Teknokona. Watu wengi wamekuwa na shauku ya kuipata Android hiyo yenye sifa nyingi mpya ikiwemo uwezo wa kuua simu inapoibiwa na muonekano wa ‘material design’ ambao unaleta hisia tofauti na ya kipekee katika utumiaji.
Kampuni chache zimeshatoa masasisho yao ya Lollipop kama LG, Motorola na Sony huku Samsung, Huawei na wengineyo wakiendelea polepole kuisukuma kwenye simu zao kadhaa.
Wiki iliyopita, kundi la Cyanogenmod wametangaza kuwa unaweza kupata jaribio lao la Android 5 na kuipakia kwenye simu au tableti yako. Kutokana na makala yao wanasema kuwa wana imani kubwa kwamba jaribio lao limekamilika kwa asilimia 85 na hivyo kuwa tayari kabisa kwa kupakia kwa vifaa kadha. Kufuatia tangazo hili, kama wewe ni mtundu wa androidi tayari umeshajua la kufanya ili kuipata.
Kupata Android mpya na kuipakia kwenye simu au tableti yako, inakupasa ujifunze kwa mtu au kusoma makala tofauti za ‘rooting android’ ambazo zitakupa ufahamu wa mchakato wa ‘rooting’ ambao unabadili ruhusa ili uweze kutoa ule mfumo ambao Samsung, Huawei na wengine wameuweka kwenye simu yako na kuweka wa kwako mpya. Chukua tahadhari juu ya mchakato wa rooting kwanza! Rooting ni jambo la hatari. Mchakato huu unaweza ukaharibu kabisa kifaa chako, iwe ni simu au tableti na kuifanya ife, isiweze kutumika kabisa, hivyo-basi kabla ya kuanza na mchakato wa rooting, inafaa ujue fika unachofanya au umtafute mtu unayemuamini akufundishe au mtaalamu akufanyie kazi hii.
‘Rooting’
Mchakato huo huanza kwa kushusha faili la ‘saferoot’ na kulipakia kwenye kompyuta. Kisha, unaunga simu yako kwa USB na kuhakikisha imeruhusu kompyuta kuiamuru kufanya mambo ya kiufundi kupitia USB (enable usb debugging). Kisha, fungua programu husika kubadili ruhusa za simu. Kama kila kitu kitakuwa shwari basi uvumilivu unahitajika ili kompyuta imalize kufanya yake kwenye simu. Ikimaliza, ujumbe utatokea kukujulisha juu ya hilo. Kama kipengele hiki kikifanikiwa, jambo moja la msingi utaloweza kufanya ni kupakia programu ya ‘recovery manager’ kwenye boot sector. Hii programu itakuwa ya kwanza kuanza unapowasha simu au tableti na hivyo kukupa uwezo wa kupakia mfumo-endeshaji wa chaguo lako. Recovery manager mojawapo inayopendwa na watu wengi ni twrp recovery. TWRP ni rahisi kuielewa na kuitumia. Pakia hii programu kwenye kifaa chako kwa kutumia maelekezo yaliyokuja na programu uliotumia ku-root.
Ukifanikiwa kuweka TWRP, zima simu yako na iwashe. Twrp itaanza na kukupa maelekezo ya kubonyeza kitufe cha kuwasha simu mara kadhaa ili kuingia kwenye chzguzo za kubadili mfumo. Ingia kwenye back-up na uhifadhi mfumo uliopo. Kisha rudi kwenye menu kuu na ingia kwenye ‘install rom’. Elekea uliloweka faili la mfumo wa android 5.0 ulioshusha kutoka cyanogenmod. Lichague n bofya flash device, kisha vuta subira mpaka imalize kupakia. Zoezi hilo likifanikiwa, unaweza kubofya return to system na simu yako itazima, itawaka na kuelekea kwenye mfumo wako mpya wa android 5.0.
Tunategemea kwamba utachukua tahadhari na utafanikiwa kufanya hili zoezi kwa umakini. Kumbuka unaweza kuungana nasi pamoja na wapenda teknolojia wenzako wengi kupitia kurasa yetu ya facebook, twitter na instagram na pia kwa barua pepe teknokonatz@gmail.com
No Comment! Be the first one.