Kuna app inayotoa huduma ya kuchati inayokuja kwa kasi sana siku hizi, inaitwa Telegram. Je ni bora kuliko WhatsApp? Leo fahamu tofauti zake kuu na ubora kati ya apps hizi mbili maarufu katika eneo la kuchati.
Urahisi katika kutumia
Apps zote mbili ni rahisi sana kujiandikisha kwani zinatumia namba yako ya simu katika kujiandikisha na kisha kutumia namba za marafiki ulizonazo katika kuongeza watu unaoweza kuwasiliana nao katika huduma zao.
Idadi ya Watu
WhatsApp inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi, kwani hadi sasa ina watumiaji zaidi ya bilioni moja wakati Telegram ina watumiaji kati ya milioni 50 hadi 70, ila wanazidi kupata watumiaji wapya kwa kasi kwa sasa.
Jambo ili linafanya uamuzi wa kuhamia Telegram kuwa mgumu kwa wengi na unakuwa rahisi pale tuu utakapoweza kuwafanya wengi wa unaowasiliana nao wao pia kutumia app hii katika simu zao.
Usalama
Ingawa app ya Telegram si maarufu sana kufikia WhatsApp app hii ndiyo salama zaidi ukilinganisha na WhatsApp. Kupitia utumiaji wa teknolojia za hali ya juu kiusalama (MTProto protocol) mawasiliano katika app hii ya Telegram ndiyo yapo salama zaidi dhidi ya wizi au uchunguzi wa kimawasiliano. Hali hii imewafanya hadi watengenezaji wa app hii kutenga zawadi ya takribani milioni 400 kwa mtu yeyote atakayeweza kushinda usalama wa app hiyo.
Pia uwezo mwingine mkubwa zaidi kiusalama katika app hiyo na uwezo wa meseji kujifuta kila baada ya sekunde au dakika flani kulingana na jinsi uliweka mipangilio (Setting) kwenye chati zako na mtu husika. Hii inamaana kama unamazungumzo ya siri na mtu basi unaweza weka hali itakayofanya mazungumzo kuwa yanajifuta kila baada ya muda mfupi baada ya kusomwa na mtu mwingine,
Kasi katika utendaji kazi
Uwezi kuamini ila Telegram ndiyo app inayofanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi ukilinganisha na WhatsApp. Hali hii inaweza ikawa inatokana na wingi wa wateja kwa huduma ya WhatsApp, ila kwa sasa fahamu ya kwamba meseji za zinazotumwa kutumia Telegram zinafika haraka zaidi ukilinganisha na kwenye huduma ya WhatsApp.
Uwezo wa kupiga simu
Uwezo huu haujafika bado kwa app ya Telegram. Kwa sasa ni app ya WhatsApp tuu ndiyo yenye uwezo wa kupiga simu.
Uwezo wa Makundi (Groups)
Apps zote zinatoa huduma za watumiaji wa app hiyo kuchati katika makundi. Wakati app ya WhatsApp inaruhusu hadi watu 100 kushiriki katika kundi moja app ya Telegram inaruhusu hadi watu mia 200 kushiriki katika kundi moja.
Uwezo wa Kutumiana Mafaili
Apps zote mbili zinaruhusu watumiaji kutumiana mafaili ya aina mbalimbali kama vile picha n.k. Wakati WhatsApp inaruhusu mafaili ya ukubwa wa hadi MB 16 app ya Telegram haina kikwazo cha ukubwa wa mafaili yanayoweza kutumwa kupitia huduma hiyo. Pia WhatsApp wananyima utumwaji wa baadhi ya aina ya mafaili lakini Telegram hawazuii, unaweza kutuma mafaili ya aina mbalimbali bila shida yeyote.
Gharama za Huduma
Wakati baada ya muda lazima ulipie huduma yako ya WhatsApp ili uendelee kutumia waanzilishi wa Telegram wamesema hakuna mpango wowote wa kulipisha watumiaji wake. Gharama zote za uendeshaji wa app hiyo unalipiwa na bilionea anayemiliki app hiyo na wamesema ata pale watakaposhindwa basi wataona ni bora waruhusu watu mbalimbali kuchangia gharama za uendeshaji wa app hiyo ila kamwe hawataonesha matangazo au kulipisha watu.
Kama ulivyoona kitu kikubwa katika WhatsApp ni umaarufu wake tayari kwa kuwa na watumiaji wengi zaidi na uwezo wa kupiga simu ila kwa kiasi kikubwa unaweza kufanya mengi zaidi kupitia Telegram.
Je, umefurahishwa na uchambuaji huu kuhusu tofauti na uwezo spesheli wa apps hizi? Tueleze wewe unatumia app gani zaidi katika masuala ya kuchati na je unapendezwa na nini zaidi katika apps hizo?
Pata Telegram -> Android – Google Play | iOS – App Store | Kwenye Kompyuta – Faili la Windows
One Comment