Raha ya teknolojia ndio hii hapa! Teknolojia inakuwa na taifa linaamua kukua nayo. Teknolojia hii inaweza ikawa inajulikana sana kwa simu na vifaa vingine vya kiteknolojia, lakini malipo? Mmmh!
Makampuni kama vile Apple na Google yanaweza yakawa yamepata mshindani mkubwa sana kama teknolojia hii ikiteuliwa kama njia rasmi ya malipo huko nchini Japan.
Kwa sasa serikali ya japan imejipanga katika kufanya majaribio ya teknolojia hiyo katika miezi ya hivi karibuni. Teknolojia hii itahusisha vidole katika mikono miwili ya mtu kuweza kuhakikiwa na mashine katika mchakato mzima wa malipo.
Katika hatua ya majaribio inayotegemewa hivi karibuni inatarajiwa kujumuisha maduka 300, mahoteli, migahawa na sehemu nyingine nyingi
Watu ambao wataanza ijaribu teknolojia hiyo ni wale ambao wanatokea sehemu za Kamakura, Shizuoka Prefecture, Kanagawa Prefecture na Hakone. Maeneo haya hayakuchaguliwa tuu kwa kubahatisha au bila sababu ya msingi. Maeneo yote hayo yamechaguliwa kwani ni sehemu ambazo zinapendwa sana na watalii katika nchi.
Sababu kubwa kabisa ambayo inaifanya serikali ya Japan kuanzisha teknolojia hii na kuifanyia majaribio ni kwamba wanatarajia kuongeza namba ya watalii ifikapo mwaka 2020. Namba hiyo inatarajiwa kuongezeka mpaka milioni 40, ambapo kwa mwaka huo mashindano ya Olympic yatakuwa yanafanyika.
Njia hii ya malipo ambayo imejikita sana katika teknolojia itawavutia watalii wengi. Kumbuka licha ya kuwa teknolojia hii itakuwa inatumika katika swala zima la malipo lakini ina uwezo wa kumtambua mtu. Hali hii inaweza ikawa inaondoa ule usumbufu wa watalii kutembea na ‘Passport’ zao wanapokuwa katika mitaa ya Japan.
Huduma hii pia itakuwa inahusisha ofa ya kutokatwa kodi mara moja kwa watalii ambao wataigia Japan. Ili mtalii kuipata ofa hii itambidi ajaze taarifa zake za muhimu kipindi ambacho anawasili katika uwanja wa ndege wa japan. Akishajiunga tuu na huduma hiyo basi vidole vyake vitaanza kuhifadhi taarifa zake muhimu kama vile zile za akaunti yake ya benki.
Kingine kizuri ni kwamba taarifa hizi zitakuwa zikikusanywa na kusimamiwa katika kuangalia mtalii anatumia pesa zake katika maeneo gani. Kama jambo hili likafanikiwa kupendwa na watalii basi bila shaka litazidi wajaza watalii katika nchi ya Japan.
Cha muhimu cha kuweka akilini ni kwamba kujiunga na huduma hii kwa watalii sio lazima, mtu unaweza ukakataa na kutumia huduma nyingine (ya malipo ya kawaida)
Kumbuka hapa katika teknolojia hii Japan inaweza ikapata changamoto kwa baadhi ya watu kutotaka kabisa kusikia kuhusu jambo hili, kwani kuna watu ambao hawapendi kutoa taarifa zao za ndani kama vile kuikabidhi nchi ya kigeni taarifa zao za alama za vidole.