Mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na ujio wa simu ya mkunjo kutoka Samsung, hatimae wahusika wamedokeza namna itakavyokuwa.
Kampuni hiyo imekuwa ikifanyia kazi wazo la utengenezaji wa simu ya aina hiyo kwa miaka kadhaa. Taarifa zaidi kuhusiana na simu hiyo itatolewa mwezi ujao kwenye mkutano wa mwaka wa wakuzaji wa bidhaa za Samsung 2018 (SDC 2018) utakaofanyika San Francisco, Marekani.
Hata hivyo, simu hiyo inaweza isiwe tayari kutolewa sasa hadi mwaka ujao 2019. DJ Koh, rais na Kiongozi Mkuu Mtendaji wa Samsung kitengo cha simu za mkononi, ndiye aliyegusia baadhi ya dondoo kuhusiana na simu hiyo wakati wa tukio la uzinduzi wa Galaxy A9 jijini Kuala Lumpur.
Simu hiyo itakuwa na muunganiko wa bidhaa mbili kwa pamoja ambazo ni tabiti na simu janja. Koh hakuthibitisha juu ya sifa mahsusi za kioo ingawa itawezekana kutumia simu hiyo kama tabiti wakati itakapofunguliwa au simu janja pindi ikikunjwa.
Umbile la nje la simu hiyo litakuwa na uwezo wa kuficha skirini yote wakati simu hiyo inapofungwa. Na hata baada ya kufungwa simu itakuwa bado ina uwezo wa kutumika huku ikitumia kioo cha nje.
Inaelezwa kuwa ukubwa wa simu hiyo utakuwa ni inchi 7.3 huku mfumo wake ukiwa ni wa OLED na pia skirini ya nje ikiwa ya vipimo vya inchi 4.6, mfumo wake wa kuonyesha picha ukiwa ni wa OLED.