Teknolojia inazidi kuwa tamu zaidi. Baada ya Microsoft kukubali kuwekeza nguvu zake kwenye programu-endeshaji nyingine za Apple na Google, sasa inaonekana Google nao wanaenda upande wa pili na kujiweka moja-kwa-moja kwenye biashara inayoiweka Microsoft juu zaidi kwa kutangaza ‘Plugin’ ya Drive kwenye Microsoft Office.
Watu walio makini na wanaofuatilia mwenendo wa huduma za hifadhi-pepe watafurahia sasa kusikia ya kwamba, wanaweza kufungua nyaraka (iwe ni ‘word’, ‘spread-sheet’ au ‘presentation’) iliyopo kwenye huduma ya Google Drive moja-kwa-moja kwenye programu ya MS Office kwa kutumia Google Drive Plug-in. Ukibadili kitu chochote kwenye nyaraka yako na Office, itajihifadhi yenyewe kwenye hifadhi-pepe ya Google Drive.
Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, tuliandika hapa Teknokona kwamba Google ilitoa kisaidizi cha kivinjari cha Chrome kinachokupa uhuru wa kufungua nyaraka yoyote kwa kivinjari hicho bila ya kuhitaji MS Office. Hatahivyo, kampuni ya Google sasa inasema kwamba kwa kutoa ‘Plug-in’ hii mpya, wanafungua milango zaidi ya huduma yao ya hifadhi-pepe ya Google Drive, kwa kukupa uhuru wa kutumia programu ambazo tayari umezizoea na unazipenda.
Hii hatua inakuja kwa sababu Google wanajua kuwa kuna ushindani mkubwa kwenye biashara ya hifadhi-pepe kwani Dropbox na Box, kampuni maarufu za huduma hizi tayari wameingia ubia na Microsoft kuweka huduma zao kama chaguo la kwanza sambamba na Onedrive ya Microsoft kwenye programu ya MS Office kwa kila mtu.
Kuanza kutumia Google Drive Plug-in, ishushe -> hapa.
Je, unatumia hifadhi-pepe kuendesha kazi zako za kila siku? Hii habari inakugusaje? Tuungane kwenye mazungumzo hapo chini.
Chanzo: GoogleForWork
No Comment! Be the first one.