Kampuni mpya ya mtandao wa simu ambayo ata bado haijaanza kutoa huduma rasmi inazidi kuonekana tishio kwa wengine kwani haipiti muda bila kusikia habari kuhusu mtandao huu mpya. Leo tutakuambia kwa nini mtandao huu una uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika ushindani katika eneo la biashara na huduma ya mawasiliano ya simu Tanzania.
Kwanza tujikumbushe Viettel ni kina nani?
Tulishaandika kuhusu mtandao huu tokea taarifa za kuja kwao zilivyoanza kusikika rasmi, Viettel ni kampuni ya mtandao wa simu wenye makao makuu nchini Vietnam. Nchini Vietnam huu ni mtandao ndiyo namba moja nchini humo na unamilikiwa na serikali ya nchini humo kupitia Wizara ya Ulinzi wa nchi hiyo. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili tayari kampuni hiyo ishaingia kwenye nchi zingine zaidi ya 3 na hii ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mataifa yote iliyoingia.
Tuhuma za Kuhujumu Miundombinu ya Wengine…
Serikali kupitia Waziri Makame Mbarawa imepinga vikali tuhuma ya kwamba mtandao huu mpya unahujumu (haribu kwa kukusudia) mitambo ya wapinzani wake kwa sasa ambapo bado ipo katika utengenezaji wa mitambo yake nchini kote.
Waziri ametoa sifa kubwa kwa mtandao huu ya kwamba utawasaidia kwa kiasi kikubwa ata wale ambao wapo vijijini kutokana na kampuni hiyo kujikita kuhakikisha wanajenga minara yao maeneo mengi zaidi hii ikiwa ni mijini na vijijini. Hii ikiwa na baadhi ya maeneo ambayo hayajawahi kufikiwa na mitandao mingine ya simu.
Kuna mfuko wa kuchangia maendeleo ya mawasiliano vijijini unaolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa makampuni ya simu pale wanapotaka kutengeneza miundombinu ya mawasiliano vijijini kwa kutambua ya kwamba huko kuna watumiaji wachache na hivyo kuchelewa kwa upatikanaji wa faida ya uwekezaji huo, inaonekana bado mitandao mingi ya simu haikutaka kutumia nafasi hii na sasa Viettel wanaitumia.
Je ni kweli mtandao wa Viettel unafaa kuogopeka?
Vyanzo vingi vinasema tayari mitandao mikubwa ya simu Tanzania, yaani Vodacom, Airtel na Tigo tayari wanakuna vichwa na kuhaha kuona ni jinsi gani kila mtu anajiweka katika mazingira mazuri ya kutoathirika na kuja kwa kampuni hii mpya ya simu.
Tuanzie nchini Vietnam…
Nchini humo mtandao wa Viettel unapatikana kwa takribani asilimia 98% ya maeneo yote yenye watu, hii ikimaanisha ni vigumu kwenda sehemu na ukapata shida ya network…wapo pande zote. Na karibia minara yao yote inarushwa signal za teknolojia ya haraka ya intaneti ya 3G (wana minara 32,000 ya 3G nchini humo).
Nchini East Timor….
Mwaka jana waliingia nchini East Timor na baada ya miezi sita wakawa tayari mtandao wao unawafikia zaidi ya asilimia 96 ya wananchi wa nchini humo. Na ndani ya mwaka mmoja wakawa wamefikisha zaidi ya watumiaji laki 5 kwa mtandao huo.
Nchini Cameroon….
Wameingia nchini Cameroon mwezi wa kumi na mbili mwaka jana na ndani ya miezi minne tuu walifanikiwa kupata watumiaji zaidi ya milioni moja kwa mtandao wao na wakisifika sana katika huduma ya intaneti ya 3G kila kona.
Msumbiji (Mozambique) je?
Walipata leseni rasmi mwezi wa kwanza mwaka 2011, na kuanza kazi rasmi kufikia kati kati ya mwaka 2012…mwaka mmoja baadae tayari mtandao huo ukawa unapatikana kwa zaidi ya asilimia 85 kwa watu wote nchini humo…na network yao ikiwa imefunika nchi nzima kwa asilimia 80% na kuhakikisha takribani watu 600,000 wakipata network za mtandao wa simu katika maeneo yao kwa mara ya kwanza katika maisha yao. Nchini humo wanatumia jina la Movitel na tayari wanashikilia nafsi namba moja kwa mtandao wenye watumiaji wengi zaidi nchini humo, wana wateja zaidi ya milioni 5.
Burundi…
Wanatumia jina la Lumitel nchini Burundi na sasa na ndani ya mwezi mmoja toka kuanza kutoa huduma walifanikiwa kuandikisha wateja 600,000…NDANI YA MWEZI MMOJA kumbuka!
Na sasa Tanzania…
Kwa kiasi kikubwa kuna uwezekano mkubwa sana wa wao kufanya vizuri sana. Kwani kwa sasa ingawa ni miezi imepita tokea tuanze kuwasikia hawajaanza kutoa huduma ila wanajiweka sawa kwa kujenga miundombinu nchi nzima wakiwa na lengo la kuanza huduma wakiwa tayari unaweza kupata huduma zao nchini kote. Na hapa ndio tunaona wamefanya cha maana sana.
Na pia nguvu yao nyingine itakuwa katika huduma ya intaneti ambapo wao wanakuja na huduma ya 3G moja kwa moja, hii ina maanisha hautakuwa na wasiwasi wa kupata huduma ya 2G ukiwa mikoani…ndani ndani hivi.Tusubiri tuone, ila na uhakika kuna mabadiliko makubwa katika ushindani yatatokea miezi michache baada ya Viettel kuanza kutoa huduma zake rasmi.
Soma Pia – Fahamu Tofauti Kuu Kati ya Teknolojia za 2G, 3G, 4G n.k
Mitandao ya simu iliyopo inatakiwa kuendelea kukuna kichwa na kuhakikisha inaboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kabla jamaa hawajaanza kutoa huduma rasmi…na hapa muda ndio huu unaisha kwani ndani miezi miwili mitatu ijayo huduma za hawa jamaa zinaweza anza rasmi. Kizazi cha sasa hivi kubadirisha laini haichukui muda sana hasa kama kufanya hivyo kutahakikisha unapata huduma bora zaidi.
[socialpoll id=”2280053″]
Habari ya kazi admin,nomba kuuliza simu yangu inaniandikia mara kwa mara maneno haya(location server error) kwenye screen je titizo ni nini, hii ni huawei 330