Australia wiki hii imeingia mkataba na Ufaransa kutengeneza Nyambizi kumi na mbili mpya, mkataba huo ambao umezua maswali mengi kwa wanaharakati nchini Australia utaigharimu nchi hiyo dola za kimarekani bilioni 50.
Japani pamoja na Ujerumani pia ziliogombea kupata zabuni hiyo lakini zikaangushwa na kampuni kutoka Ufaransa ambayo ndiyo itatengeneza nyambizi hizo ambazo mpaka mwaka 2030 ndio ya kwanza itakuwa tayari.
Nyambizi hizi ambazo ni za aina ya shortfin zitajengwa katika pwani ya kusini mwa Australia, inategemewa mradi huu utatengeneza kazi mpya karibu 2800. Chuma kitakachotumika kujenga nyambizi hizi ni chuma kinachopatikana Australia na wafanyakazi watakao tumika kwa kiasi kikubwa ni raia wa Australia.
Australia kijiografia imezungukwa na maji kitua mbacho kinawapa haja ya kuwa na nyambizi kwaajiri ya kufanya doria katika bahari zake, lakini pia majirani wa taifa hili wamekuwa wakiongeza maradufu uwezo wa majeshi yao kwa hivyo nyambizi hizi zitakuwa ni moja ya hatua za kuongeza ushawishi wao katika eneo hilo la asia ya mashariki.
Pamoja na kujiongezea nguvu kama taifa, hifadhi ya nyambizi ilizonazo Australia kwa sasa ni za aina ya zamani ambazo zimepitwa na wakati hivyo makubaliano hayo na kampuni ya DCNS ya Ufaransa itatengeneza nyambizi mpya na za teknolojia ya kisasa. Shortfin ni aina ya nyambizi ambazo zinasifika kwa kuwa na maboresho katika teknolojia yanayozifanya ziende kwa ukimya zaidi (moja ya sifa muhimu kwa nyambizi) lakini pia zinauwezo mkubwa wa kugundua chombo cha adui.
Inasemekana kwamba moja ya sababu ambazo zinaweza kuwa zimesababisha nchi ya Japani kukosa zabuni hii ni kukosa uzoefu katika kuuza vifaa vya kijeshi nje ya nchi kwani huko nyuma katiba ya nchi hiyo haikuruhusu Japani kuuza vifaa vya jeshi nje ya nchi na hii ingekuwa ndiyo zabuni ya kwanza kubwa kushinda baada ya kubadilisha sheria zao kuruhusu biashara ya vifaa vya jeshi nje ya nchi.
Makala hii imeandikwa kwa msaada BBC na mitandao mingine iliyoripoti habari hii.