Je ni sifa gani za kuangalia katika kununua laptop kwa matumizi ya mwanafunzi wa chuo? Katika ulimwengu wa sasa ni muhimu kwa mwanafunzi wa elimu ya juu kuwa na kompyuta hasa hasa ya laptop.
Kuna mara kadhaa katika muda wake wa mafunzo atakapojikuta kuna vitu ili vifanyike basi ni lazima kompyuta itumike.
Kompyuta ya mwanafunzi ina sifa gani? Kikuu ni kuwa na kompyuta itakayokusaidia katika majukumu yako ya kila siku, katika makala hii tutakuonesha sifa kadhaa za kuziangalia pale unapotaka kununua laptop kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu mwingine anayeingia chuoni n.k.
Katika suala la bajeti linategemea mambo mengi sana lakini kwa sifa hizi tunazokupa unaweza kukutana na kompyuta zinazoangukia bei kati ya Tsh 550,000/= – 900,000/= | Kes 27,000/= – Kes 40,000/=. Ukiwa mjanja na kama ni kompyuta (laptop) iliyokwisha tumika basi utaweza pata dili zuri zaidi kipesa.
Je ununue inayotumia Ubuntu, Windows au Mac OS?
Hapa kwa kiasi kikubwa kompyuta inayotumia Windows itafaa. Laptop zinazotumia programu endeshaji ya Ubuntu zinakuwa zinauzwa kwa bei nafuu zaidi lakini bado inaweza msumbua mwanafunzi katika utumiaji wake kama itakuwa ni mara yake ya kwanza. Ila njia nyingine ni kununua na kisha kuweka programu endeshaji ya Windows mwenyewe.
Je iwe na ukubwa wa kiasi gani wa Diski Uhifadhi (Storage)?
Kwa mwanafunzi tunaamini kitu muhimu sana ni masuala ya kutafuta mambo mtandaoni, kusoma na kuandika document mbalimbali, hivi vyote havihitaji kiwango kikubwa sana cha diski uhifadhi.
Tukifikiria ya kwamba lazima atataka kuwa na muziki na filamu mbili tatu ndani yake basi kiwango cha GB 250 – GB 500 ni kiwango kinachotosha tuu.
Ila kumbuka ujazo si kipaumbele sana siku hizi, ni bora uchague laptop yenye kiwango cha juu zaidi cha RAM na CPU… kwani suala la diski uhifadhi kama kiwango ni kidogo basi utaweza kutumia ‘external disk’.
Je iwe na ukubwa na uzito gani?
Kompyuta ya upana wa inchi 11 had 14 ni sawa kabisa kwa matumizi ya kishule. Ila pia haitakiwi iwe nzito sana, kumbuka kuna kuibeba beba na kuhama na hivyo ikiwa nzito sana inakuwa katika hatari ya kukuponyoka muda wowote.
Kipimo kizuri cha upana kinategemea sana ukubwa wa mwili wa mtumiaji, mwenye mwili mdogo anaweza akatumia kwa pozi zuri laptop yenye ukubwa mdogo wakati mwenye mwili mkubwa kompyuta hiyo hiyo itakuwa ni kichekesho kwake. Hataweza kuandika/kutumia kwa raha.
Betri…..ikae na chaji kwa muda gani kwa wastani?
Chagua laptop yenye uwezo wa kukaa na betri kwa zaidi ya masaa 6 kwa matumizi ya kawaida. Katika maisha ya kila siku ya chuo mwanafunzi anaweza jikuta hajafanikiwa kukaa sehemu ya kumuwezesha kuchaji mara kwa mara.
Vipi kuhusu sifa zingine kama vile RAM, CPU?
Hapa ni vizuri kuchagua ya si chini ya GB 2. Kama bajeti inaruhusu ni vizuri kuchukua yenye kiwango cha GB 4 au zaidi. Kwa kiwango hichi utaweza kufungua mafaili kadhaa bila laptop yako kuanza kujivuta katika kufanya kazi.
CPU – Hapa patategemea zaidi bajeti yako. Laptop zenye CPU za Pentium na Celeron ni za bei nafuu zaidi lakini si CPU bora zaidi.
Kama bajeti inaruhusu basi chagua kompyuta yenye prosesa ya familia ya Intel tena toleo la 5 (5th Generation Core processors/Broadwell). Hapa namaanisha laptop zinazotumia Core i3 na kama pesa ni nzuri basi Core i5 au i7.
Kwa bei nafuu ila uwezo wa kazi unaokaribiana na hizo za Intel 5th Gen basi chagua zinazotumia AMD. Ila ubaya wa zinazotumia CPU ya AMD ni kwamba zinatumia kiwango kikubwa zaidi cha chaji ukilinganisha na Intel.
Vipi kuhusu Keyboard na ‘Touchpad’?
Usiishia kuulizia kiwango cha RAM, Diski Ujazo na CPU tuu, kingine muhimu ni kiwango cha ubora wa Keyboard na eneo la ‘Touchpad’.
Kama kiwango cha ubora wa keyboard ni mbaya basi mtumiaji atakuwa anaandika kwa shida, pia kama Touchpad nayo si bora basi mtumiaji atapata shida sana katika utumiaji wa laptop husika.
Vingine muhimu;
Hakikisha kuna ports za kutosha za USB (Mbili au zaidi), pia HDMI na port nyingine yeyote unayoona ni muhimu kulingana na mahitaji.
Display – Wachache huwa wanaliangalia sana hili. Kiwango cha pixel cha kwenye display ni muhimu sana katika suala la ubora wa mtazamo. Display yenye kiwango cha pixel cha 1366×768 au 1600×900 au zaidi ya hapo ni bora zaidi.
No Comment! Be the first one.