Watumiaji kadhaa wa simu zinazotumia Android wameripoti kuhusu picha inayoharibu simu. Yaani picha hii inaweza ‘kuzingua’ ufanyaji kazi wa simu yako.
Picha hii inayoonesha ziwa, anga ya jioni na pwani inasababisha simu kushindwa kufanya kazi pale ikitumika kama wallpaper – picha kuu ya eneo la apps/nyumbani.
Je ni simu gani zinazopata shida?
Inasemekana watumiaji wa baadhi ya simu za Samsung na zile za Google Pixel ndio wanaoathirika zaidi ingawa pia kuna baadhi ya simu zingine pia zinazoathirika.
Kinachotokea ni pamoja na simu kuanza kuzima mwanga na kujiwasha tena eneo la kioo kikuu/screen, hii pia ni pamoja na kuifanya simu kuwa nzito na hivyo ata kushindwa kutumika.
Jinsi ya kutatua
Ingawa kama utaweza kufika eneo la settings/mipangilio na kubadili wallpaper kwa kuweka nyingine basi utaweza kutatua tatizo. Ila kwa wengi hali inayoletwa na utumiaji wa picha huo kama wallpaper na hivyo kumfanya mtu kushindwa kabisa kwenda eneo la kubadili wallpaper.
Katika hali kama hiyo njia pekee ya kuweza kuitumia tena simu yako ni kufanya ‘factory reset’ – yaani kuformat simu na kuirudisha katika upya wake.
Inasemekana tayari Samsung anafanyia kazi kuhakikisha kuna sasisho/update la Juni 11 litakalotatua tatizo hilo.
Je inakuwaje picha hiyo kusababisha tatizo hilo?
Kikubwa ni kwamba simu yako ili kuonesha rangi za picha n.k inahusisha prosesa ya simu yako kuzisoma data za picha husika na ndio kuweza kuonesha kile inachotakiwa kuonesha. Mchanganyiko wa aina za rangi katika picha hii inasemakana umeweza sababisha prosesa nyingi za simu kujichanganya na hivyo kushindwa kusimamia vizuri kazi au mahitaji mengine ya simu kiutendaji.
Tunakushauri usijaribu kuiweka picha hii kama Wallpaper, ila kwa wale wazee wa kujaribu kila kitu usisahau kutuambia unachokutana nacho unapotumia picha hii.
Vyanzo: XDA, Twitter na vyanzo mbalimbali