Katika dunia ya leo, wewe kama msomi au mtu makini, unapaswa utambue na utumie mifumo bora ya kutunza kumbukumbu na mawazo muhimu. Inawezekana tayari unatumia picha, sauti na video kutunza kumbukumbu zako ila, je, una mfumo unaokuwezesha kuziweka kwenye makundi yanaoshabihiana au kuzifanya uzipatikane popote ulipo na kwenye kifaa chochote ulichonacho?
Teknolojia ya sasa inakupa urahisi wa kutunza na kupangilia kumbukumbu muhimu, kiasi kwamba ni ngumu kuzipoteza.
Karatasi na Mbinu za Kisasa
Karatasi zimetumika kwa muda mrefu kwenye utunzaji wa kumbukumbu na hilo jambo halionekani kuisha. Utumiaji wa karatasi una changamoto zake, kama ulazima wa kuzibeba na nafasi na uzito mkubwa unaochukua zikiwa nyingi. Pia, karatasi zina uwezekano wa kuharibika na hata kuibiwa, usizipate tena.
Watu wengi hawawezi kuacha kutumia karatasi kutunza kumbukumbu na mawazo yao kwa sababu ya urahisi wa kuzitumia kufanya kazi na kuwasiliana. Karatasi hizi zinaweza kuingizwa kwenye kitumi, kama simu janja kwa njia ya kamera ili kuzitunza.
Tumia programu Maalumu za Unakili
Haitoshi kupiga picha maneno yako na kuyahifadhi kwenye simu kama picha nyingine za kawaida. Unaweza kuzibadili kuwa nyaraka za pdf kwa matumizi ya kazini ila kwa matumizi binafsi, tumia ‘app’ au programu muhimu kwa ajili ya kutunza mambo unayoyanakili (note-taking apps). Kwa kawaida simu janja nyingi huja na programu kama hizi. Apps hizi zinakupa uhuru wa kawaida sana wa kutunza kumbukumbu.
Jaribu kuona kama zinakurusu kuingiza picha kwenye maneno unayonakili. Kama hazikupi uhuru huo, unaweza kutafuta programu mahsusi zaidi kama Evernote, OneNote na Google Keep, ambazo zinakupa uwezo mkubwa zaidi wa kutunza na kupangilia notes, picha, sauti na video katika sehemu moja. Kama unahitaji uwezo maradufu, zipo simu za aina ya Samsung Note, zinazotengenezwa mahsusi kwa ajili ya kutunza na kushughulika na kumbukumbu muhimu.
Uwezo Zaidi
Programu kama Evernote, OneNote na Google Keep zinakusadia uondokane na adha na aibu ya kusahau mawazo yako na kumbukumbu muhimu. Ijulikane wazi kwamba hizi programu siyo za kuweka nyaraka muhimu (‘Important Documents’) kwani siyo kazi yake. Kazi yake ni kuweka kumbukumbu na mawazo muhimu kwako.
Uzuri wa hizi programu mahsusi zaidi ni uwezo mkubwa wa kuhifadhi, urahisi wa kupata kumbukumbu zako kwenye vitumi tofauti na uwezo wa kufanya kazi pamoja na watu wengine juu ya mawazo yako. Programu hizi hutumia akaunti maalumu kukutambua na taarifa zako kuweza hata kukukumbusha ukamilishe wazo unalofanyia kazi.
Kama unajisikia uvivu kuandika, programu hizo zinakupa uwezo wa kunakili maneno kwa kuyaongea kwenye simu na kompyuta, au hata kuyanyakua kutoka kwenye muandiko wako kutoka kwenye karatasi uliyoipiga picha. Pamoja na hayo, kuna mambo mengine lukuki ambayo programu hizi zenye uwezo wa ziada zinaweza kufanya.
Ni Dhambi
Huu ni wakati wa kuwa mjanja zaidi kwa kutumia teknolojia. Tumia karatasi kama kawaida ila tumia kamera, kinasa sauti na programu kama Evernote, OneNote na Google Keep kuongeza ufanisi kwenye kufanya kazi zako. Itakuwa ni dhambi kisayansi kama utatumia kisingizio cha kusahau au kupoteza mawazo na kumbukumbu zako tena.
Tujuze teknokona kuhusu ujanja wako pia!
No Comment! Be the first one.