Elon Musk na Mark Zuckerberg wana vitu kadhaa wanavyofanana zaidi ya kuwa mabilionea. Wote wana shauku ya kuhakikisha kuwa anga inakuwa ndicho chanzo kikuu cha usambazaji na utoaji wa huduma za intaneti katika miaka kadhaa ijayo.
Ingawa kujenga uwezo wa kutumia intaneti ya anga sio jambo jipya, kinachopelekea hasa hawa jamaa kung’ang’ania jambo hili ni uwepo teknolojia mpya na unafuu wa gharama za kurusha vyombo vitakavyotoa intaneti kutoka angani.
Tarehe 1 Septemba, Amos 6 ambayo ni Setilaiti ya Facebook ililipuka wakati ilipokuwa katika kifaa cha kurusha kwenda angani. Kifaa hicho kinachojulikana kama roketi la SpaceX kinatengenezwa na kampuni inayomilikiwa na Elon Musk, bilionea ambaye ni mzaliwa wa Afrika Kusini anayeishi Marekani mwenye uraia wa nchi tatu, Afrika Kusini, Canada na Marekani.
Kusudio kubwa la kurusha setilaiti ya Facebook lilikuwa ni kutoa huduma ya Intaneti kwa nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika na ilikuwa ni kati ya mipango ya Zuckerberg ya kuiunganisha dunia nzima na intaneti.
Kwa Zuckerberg, ambaye kwa miaka kadhaa umekuwa ni mpango wake binafsi kuunganisha dunia kwa intaneti, kuharibika kwa setilaiti hiyo haikuwa habari njema hata kidogo. Katika wakati ambao amekuwa Barani Afrika, eneo Kusini mwa jangwa la Sahara kwa mara ya kwanza akizungumza na wataalamu wa teknolojia na viongozi wa serikali kuhusu mpango wake huu, lazima angesikitika vilivyo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook Mark aliandika “Wakati huu ambao nipo Afrika, nasikitika sana kusikia kuwa ilishindikana kurusha SpaceX na jaribio hilo liliteketeza kabisa setilaiti yetu ambayo ingetoa intaneti kwa wajasiriamali wengi na kila mmoja katika bara hili.”
Kwa bahati nzuri, Facebook hawajakata tamaa na hivi karibuni watarusha kifaa kingine cha intaneti angani kwaajili ya Afrika. Mark anasema “kwa bahati nzuri tumeendeleza teknolojia nyingine kama vile Aquilla (Drone la Intaneti la Facebook) ambayo itawaunganisha watu pia, bado tutaendelea na mkakati wetu wa kumuunganisha kila mmoja na tutaendelea kufanya kazi hadi siku ambayo kila mmoja atanufaika na fursa zitakazoletwa na Intaneti hii.