Wapenzi wa muvi wa nchi mbalimbali wameshangilia sana ujio wa huduma ya Netflix katika nchi zaidi wiki hii. Huduma hiyo iliyokuwa inapatikana katika nchi chache tuu sasa itakuwa inapatikana karibia ulimwenguni kote.
Kwanza Netflix ni nini?
Netflix ni huduma namba moja duniani ya kukupatia video za filamu na tamthilia kwa njia ya kuzitazama kupitia huduma ya intaneti, kimombo ‘streaming’.
Badala ya kushusha (download) utaweza tazama filamu mbalimbali mpya na za zamani moja kwa moja kwenye simu, tableti au kompyuta yako.
Je ni bure?
Hapana, kuna vifurushi kadhaa ila kifurushi cha kuanzia ni dola $7.99 (Takribani Tsh 17,504/= au Kes 816/=).
Mbona watu wanazungumzia Netflix sana siku hizi chache?
Huduma ya Netflix inakua kwa kasi sana na kwa muda mrefu huduma hiyo ilikuwa inapatikana kwenye baadhi ya nchi tuu, ila kuanzia sasa mtu yeyote katika taifa lolote anaweza kutengeneza akaunti katika mtandao huo na kufurahia huduma.
Zamani ilikubidi utumie programu spesheli za kudanganya mtandao huo sehemu ulipo kama vile Hola ili uweze kutumia huduma hiyo.
Je DSTV, Azam, StarTimes, Zuku na wengine wanasababu ya kuogopa?
Hili linategemea. Kwa kiasi kikubwa Netflix inaleta ushindani mkubwa katika eneo la filamu mpya kuwahi kuwafikia zaidi. Kumbuka Netflix inakupa chaguo kama vile unapoenda kwenye mtandao wa YouTube, unaweza chagua mwenyewe kitu gani utazame.
Wakati huduma kama vile DSTV na wengine wanaopewa lawama zaidi ya kurudia rudia filamu hasa za zamani hali kwa Netflix ni tofauti kidogo. Wanajitahidi kuwa na filamu mpya zaidi na pia kuna vipindi vingine wenyewe wanawekeza katika utengenezaji wake.
Kwa kifupi DSTV mwenye vifurushi vya bei ghari zaidi ndiye mwenye hatari ya kupoteza wateja wanaolipia vifurushi hivyo kwa sababu ya filamu kwani inawezekana gharama ikawa ndogo au karibia sawa na hiyo ya DSTV ukijumlisha intaneti ila kwa Netflix watakuwa wakipata filamu nyingi na bomba zaidi muda wowote watakao.
Kwa watu wanaopata huduma nzuri za intaneti katika mfumo wa 4G kama vile Smart, Smile na mingineyo basi wataweza kufurahia zaidi huduma hii. Lakini ukweli ni kwamba ingawa vifurushi vya Netflix ni vya bei nafuu bado wengi watashindwa kutumia huduma hii katika nchi yetu kutokana na changamoto ya upatikanaji wa intaneti ya kasi na pia gharama ya vifurushi vya intaneti ya kasi.
Kwa kifupi hakuna atakayeathirika kati ya DSTV, Azam, StarTimes na Zuku. Wote pamoja na Netflix wataendelea kupata wateja bila kuathiri kundi jingine. Ila kwa wateja wa DSTV wanaolipa pesa nyingi kwa ajili ya kutazama filamu ndio wenye nafasi kubwa zaidi ya kuachana na vifurushi hivyo vya gharama na kuhamisha pesa hizo kwenye intaneti ya kasi ili waweze kupata huduma bora zaidi katika eneo la filamu na tamthilia – Netflix.
Je kujiunga naitaji nini?
Unaitaji akaunti ya benki iliyounganishwa na huduma za malipo ya kimataifa – Visa au MasterCard. Kisha unaenda kwenye mtandao wao unachagua kifurushi unachoona bora zaidi kwako, unaingiza taarifa za kadi yako ya malipo na kama taarifa ipo sahihi basi tayari unaweza anza kufurahia huduma hiyo
Naitumiaje???
Ukishakuwa na akaunti utaweza kutumia Netflix iwe kwenye simu, tableti, kompyuta au TV janja (tv zenye apps – kuna app ya Netflix).
Kwenye kompyuta unatembelea tuu mtandao wao na utaweza kupata huduma moja kwa moja. Kwenye simu au tableti unaweza kupakua app yao.
‘Muhimu: Kama tayari unatumia huduma nyingine ya TV na unalipa pesa nyingi kila mwezi unaweza piga mahesabu ya huduma ya intaneti pamoja na malipo ya kila mwezi ya Netflix na ukajikuta bora ulipie Netflix’
Ni muhimu kuhakikisha unapata intaneti ya uhakika, kwani kama intaneti itakuwa si ya uhakika video itakuwa inacheza huku ikisimama simama – ‘buffering’
Ila Uchina ni moja ya nchi chache ambayo huduma hii itachelewa kuwafikia bado, inaonekana kwa kiasi kikubwa ni suala la sheria kali za kukubaliana nazo za nchini humo ndio zimewachelewesha.
No Comment! Be the first one.