Zipo namna tofauti za kuhifadhi vitu mtandaoni ili uvione baadae. Mitandao mingi mikubwa ina njia zake tofauti za kufanya hiyo, kama ‘favourites’ ya twitter, ‘Save’ ya facebook na ‘bookmarks’ kwenye kivinjari chako. Kwa muda mrefu, njia hizi zimekuwa zikitumika ila kwa sasa njia ya kisasa zaidi ni kutumia huduma mahsusi kama Pocket, Instapaper na Readability ambazo, mbali na kuhifadhi kurasa, huzishusha kwenye simu au tabiti yako ili usome baadae bila intaneti
Pocket, huduma kinara
Kati ya huduma tajwa, Pocket ni huduma kinara na unaweza kuiona moja-kwa-moja kwenye kivinjari cha Mozilla Firefox.
Kama hukioni kitufe hiki cha Pocket, sasisha Firefox au tafuta kisaidizi cha Pocket kwenye Firefox Add-ons.
Kwa kawaida, Pocket haipo kwenye kivinjari cha Google Chrome. Itakupasa uchukue kisaidizi cha Pocket kutoka Chrome web store.
Kama tayari, una pocket kwenye vifaa vyako, uko tayari kwa maelezo yanayofutata. Maelezo haya yanaweza pia kutumika kwa huduma nyingine za Instapaper na Readablility.
Jiunge na kubali kuingia (sign up and sign-in)
Kama ilivyo sawa na app zingine, ukitaka kufaidi zaidi Pocket, itakubidi au itakufaa (Kiswahili cha Kenya) ujiunge na huduma yake kwenye wavuti, kivinjari na simu au tabiti. Kwa sasa kuna chaguzo tatu – jiunge kwa kutumia barua-pepe ulionayo, kwa akaunti yako ya g-mail na kwa kutumia akaunti ya Firefox (kama unayo).
Peruzi na Hifadhi
Kwenye kompyuta, tumia kivinjari chako kuperuzi wavuti na ukipenda kurasa fulani kwenye tovuti yoyote, bonyeza kitufe cha Pocket kuhifadhi makala, video na/au picha. Kichaguzo kidogo kitatokea cha kuweka ‘tag’ – hii itakusaidia kupangilia kurasa zako. Kwenye simu au tabiti, tumia chaguzo ya kushirikisha (‘share’) kwenye kivinjari chochote, kisha ‘share to Pocket’.
Ukifanya hayo kurasa uliyoipenda itatumwa kwenye mfuko wako (‘Pocket’) wa kwenye wavuti na itaanza kupakuliwa kwenye simu na tabiti yako.
Soma Baadae
Ukifanikiwa kuhifadhi makala, video au picha kwa njia yoyote iliyoelezwa hapa, utaweza sasa kuingia kwenye tovuti ya getpocket.com au kufungua app ya pocket kwenye kifaa chako cha kiganjani.
Unaweza sasa kutengeneza na kuona makundi mbalimbali ya makala unazosoma kwa kutumia ‘tags’. Pia unaweza kuwekea makala fulani mkazo zaidi kwa kuzifanya ‘favourite’.
Faida za huduma za ku- soma baadae
Usikubali kupitwa na mbinu hii kuhiadhi vitu mtandaoni. Itakusaidia kuokoa muda na kupanga vyanzo vya makala zako vizuri zaidi kama mtafiti bora. Pia, baadhi ya huduma hizi huongeza urahisi wa kusoma kurasa za mtandaoni kwani hutoa kila kitu kwenye makala, ikiwa pamoja na matangazo na kuacha maneno na picha husika tu!
Hasara
Kampuni kama twitter,Flipboard, Pulse na Zite tayari zimejiweka vizuri kuitumia pocket. Huenda hii ikawa njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa watumiaji wanatumia muda mwingi kwenye tovuti zao bila ya wasiwasi wa kupitwa na habari wanazoziona juu kwa juu. Kwa maana hiyo, unaweza kujikuta unatumia muda mwingi zaidi kuhifadhi makala kuliko kuzisoma baadae kama ulivyopanga.
Kwa sasa kipengele cha kuondoa matangazo kipo kwenye kivinjari cha Firefox pekee. Kwenye Pocket ya kivinjari cha Chrome hakipo. Adha Hii inatuleta kwenye sehemu ya pili ya makala hii.
Tumia huduma ya ‘Clearly’ kwenye Google Chrome
Kama ungependelea kutumia uwezo wa kuondoa matangazo na mambo mengine kwenye kurasa ili kuongeza umakini wa kusoma kupitia kivinjari cha chrome basi sulujisho la hilo ni kutumia app ya ‘Clearly’ kutoka kampuni ya Evernote.
App hii inapatikana kwa kutumia kisaidizi cha utakacho kipata kupitia soko la chrome, chrome webstore.
Ukishaipakia kisaidizi hicho, ‘sign-in’ na tumia app hiyo muda wowote, kirahisi.
Tupe ujanja wako
Mbali na Pocket na Clearly, ambazo nimefanikiwa kutumia, kuna huduma nyingine ambazo ni maarufu na pengine umewahi kutumia kama Instapaper na Readability. Tupe maoni yako. Tujuze.
One Comment