Je wewe ni mpenzi wa filamu za Batman? Basi fahamu kampuni ya Faraday Future inayowekeza katika teknolojia ya magani yanayotumia umeme wametambulisha gari la kuvutia lenye muonekano kama gari linaloendeshwa na mhusika mkuu katika muvi za Batman.
Gari hilo walilolipa jina la FFZERO1 limetambulishwa rasmi katika maonesho ya vifaa vya teknolojia ya CES yanayoendelea jijini Las Vegas nchini Marekani.
Tajiri wa nchini China, Bwana Jia Yueting ndio muwekezaji mkubwa katika kampuni hiyo yenye takribani umri wa miezi 18. Wengi wanaamini soko la magari litahamia kwenye magari yenye mvuto na yanayotumia teknolojia za kisasa zaidi katika miaka ya hivi karibuni, na hii ni pamoja na kutumia umeme badala ya kutegemea mafuta tuu.
“Apple hawakubadilisha na kuboresha simu tuu, waligusa pia kila sehemu ya maisha yetu na sisi (Faraday Future) tunataka kufanya hilo pia”….“Tunataka kuleta mabadiliko katika nini hasa tunafikiria pale tunapozungumzia usafiri”, alisema mmoja wa viongozi watendaji wa kampuni hiyo, Bwana Nick Sampson.
Gari ili walilotumia katika maonesho ni utambulisho wao rasmi ya nini wanachoweza kufanya na wanategemea kuweza kuanza kuingiza magari sokoni ndani ya miaka michache kuanzia sasa. Kwa sasa juhudi ni katika kutengeneza kiwanda kikubwa nchini humo – tayari wanawafanyakazi 700 ila kiwanda chao kikimalizika wanategemea kuwa na wafanyakazi takribani 4,500.
Hadi sasa kampuni hii inajivunia kuvutia wafanyakazi waliokwisha fanya kazi kwenye makampuni makubwa kama vile Google, Tesla, BMW na Apple.
Wameshasema ya kwamba magari ya mwanzo kutoka kwenye kampuni hiyo yasitegemewa kuwa magari ya bei nafuu, na wengi wanategemea kuweza kupata gari kama hilo lililooneshwa lazima uwe na mabavu kwelikweli kipesa.
Ushindani unazidi kukua katika eneo la teknolojia za magari janja ya kisasa yanayoangalia utumiaji wa teknolojia kwa njia ya kitofauti zaidi ukilinganisha na magari tuliyoyazoea kila siku. Faraday Future wanaingia kwenye kundi la makampuni mengine kadhaa kama vile Google, Tesla na mengineyo.
Usipitwe na habari, jiunge nasi katika mitandao ya kijamii – Facebook, Twitter, na Instagram
Picha: Verge, LA Times, na vingine.
No Comment! Be the first one.