Kampuni ya Apple imefunguliwa mashitaka mdai akisema app yao ya iPhone FaceTime imehusika kusababisha ajali ya gari iliyotokea mwaka 2014 na kusababisha kifo cha mtoto mdogo.
Kesi hiyo imefunguliwa tarehe 23 Disemba mwaka jana, imesema kosa kubwa la Apple ni kutoka jumuisha teknolojia waliyonayo ya kuweza kuzuia baadhi ya apps kufanya kazi pale mtumiaji akiwa ndani ya chomo cha usafiri.
Tayari Apple wanamiliki hati-miliki ya teknolojia inayowawezesha kuzuia baadhi ya apps kufanya kazi pale mtumiaji akiwa ndani ya chomo cha usafiri. Wana hakimiliki (patent) ya teknolojia hiyo tokea April 2014.
Kikuu kuhusu kesi hii
Ajali hiyo ilitokea mjini Texas usiku wa Krismasi mwaka 2014. Muendesha gari mmoja ambaye alikuwa anatumia app ya FaceTime kwenye simu yake ya iPhone 6 Plus alijisahau na kujikuta akiligonga gari lililokuwa likiendeshwa na Bwana James Modisette ambaye alikuwa na mtoto mdogo kwenye gari lake. Baada ya ajali hiyo mtoto huyo alifariki dunia na polisi walipofika na kuchukua maelezo kijana aliyesababisha ajali hiyo alikubali ya kwamba app ya FaceTime ilimuondoa makini.
Kitu kikubwa zaidi ni kwamba hii kesi inahusisha Apple kuwa na uwezo wa kufanikisha teknolojia ambayo ingeweza saidia kuepusha ajali hiyo ya gari kutokea.
Familia ya mtoto huyo aliyefariki inadai Apple inatakiwa ilipe fidia kwa uzembe – kutokuruhusu teknolojia salama iliyo tayari ndani ya simu zake ifanye kazi ili kunusuru ajali za namna hii.
Tayari dereva wa gari lililosababisha ajali hiyo ana kesi yake tofauti ya makosa ya barabarani na kusababisha kifo, kesi hii ni tofauti kabisa.
Ugumu upo wapi?
Kesi hii italeta maswali mengi sana. Kama Apple wakikutwa na hatia ina maana ata huduma zingine maarufu kama vile Facebook, WhatsApp na zingine kama hizo watajikuta kwenye wakati mgumu juu ya kitu kama hicho.
Pia kuna uwezekano mkubwa teknolojia hiyo inayosemekana tayari Apple wanayo kwenye simu zao kama wakiiwesha kufanya kazi inaweza pata shida kutofautisha simu za anayeendesha gari na yule asiyeendesha gari mfano Abiria. Kuna uwezekano mkubwa wakiruhusu teknolojia hiyo ifanye kazi basi ata simu za abiria zinaweza koseshwa huduma muhimu.
Apple wamesemaje?
Hadi sasa Apple hawajasema chochote kuhusu kesi hiyo.