Kampuni ya Simu ya Huawei imeingia makubaliano na kampuni ya huduma ya kutuma fedha kwa simu ya WorldRemit kuwawezesha wateja kutoa na kupokea fedha nje ya Bara la Afrika.
Huduma hiyo itawawezesha wateja waliopo barani Afrika kupokea fedha moja kwa moja kwa njia ya simu kutoka nchi zilizopo nje ya Afrika kwa urahisi zaidi tofauti na ilivyo sasa.
Akizungumza Julai 11 wakati wa kusaini makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa Huawei, David Chen amesema hatua hiyo itasaidia kuziunganisha akaunti zaidi ya 100 milioni kupitia kampuni hiyo na kurahisisha huduma za kifedha. 

“Huduma hii ya kimataifa ni muhimu kutokana na kuwepo tatizo la kiteknolojia katika utoaji huduma za kifedha nje ya Afrika lakini kwa pamoja tunataka kupunguza vikwazo na kurahisisha huduma za kifedha,” amesema.
Mkurugenzi wa WorldRemit, Ismail Ahmed amesema kampuni hiyo inapanua wigo wa huduma zenye ubora, usalama na gharama nafuu.
“Teknolojia hii ni ya msingi na kwa kuwa inafanya kazi kwenye simu (smartphone) imekuwa na mafanikio makubwa katika kuendeleza masoko,” amesema.
chanzo: Mwananchi